• HABARI MPYA

    Saturday, August 26, 2017

    MTIBWA SUGAR YAAHIDI KUFANYA KWELI LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAKATI Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/2018 unaanza Jumamosi, klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro imepania kufanya vizuri chini ya kocha wake mkuu Zuberi Katwila.
    Beki mahiri wa klabu hiyo, Salum Kanoni Kupela aliyesajiliwa kutoka Mwadui FC ya Shinyanga  pia beki huyo wa kulia aliwahi kutumikia vilabu vya Simba na Kagera Sugar , alizungumza juu ya matarajio yake msimu ujao.
    “Nadhani kitakachotubeba ni ushirikiano na kujituma kila ninayemuona anapigania timu hivyo nadhani msimu huu tutafanya vizuri zaidi na kushika nafasi za juu, wachezaji waliosajiliwa na waliokuwepo ni wana uwezo mkubwa sana kikubwa Allah atuongoze,"alisema Kanoni.
    Beki huyo wa zamani wa Simba SC na Kagera Sugar amesifu maandalizi yao ya msimu huu kwamba yamekuwa mazuri.
    “Benchi la ufundi limekuwa likitupa mazoezi na maelekezo bora kabisa, pia tumekuwa tukijengwa kisaikolojia, hakika msimu unaoanza nawakaribisha mashabiki wa Mtibwa Sugar kuhudhuria kwa wingi uwanjani watupe ushirikiano wao, nina imani kwa pamoja tutafika mbali sana kwa kuwa uwepo kwao ni faraja kubwa kwetu," aliongeza Kanoni.
    Kanoni amesema michezo ya kirafiki waliyocheza imewasaidia kujuana na kurekebisha makosa yaliyojitokeza.
    “Tumepata michezo mingi ya kirafiki na ilikuwa kipimo tosha kwetu na michezo hii imetusaidia kutengeneza muunganiko kwa kuwa tupo wachezaji wageni na wa zamani, hivyo ili tuzoeane vizuri ilibidi tucheze michezo mingi nadhani hadi sasa tumeelewana na tuko tayari kwa msimu mpya” Kanoni.
    Mtibwa Sugar inatarajiwa kuanzia nyumbani Uwanja wa Manungu, Turiani mjini Morogoro kwa kumenyana na Stand United ya Shinyanga Jumamosi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MTIBWA SUGAR YAAHIDI KUFANYA KWELI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top