• HABARI MPYA

    Sunday, August 27, 2017

    YANGA YAANZA NA SARE, 1-1 NA LIPULI TAIFA

    Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
    MABINGWA watetezi, Yanga SC wameanza vibaya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Lipuli ya Iringa jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hans Mabena aliyesaidiwa Mohammed Mkono wote wa Tanga na Grace Wamala Kagera, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa tayari zimekwishafungana mabao hayo.  
    Lipuli walitangulia kwa bao la mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Seif Abdallah Karihe dakika ya 44 kabla ya Yanga kusawazisha kupitia kwa Donald Ngoma dakika ya 45.
    Lipuli walipata bao lao kwa shambulizi la kurudisha, wakitoka kushambuliwa na kipa Agathon Mkwando akaanzisha mpira haraka hadi kumkuta Karihe aliyekwenda kufunga.
    Beki wa Yanga, Andrew Vincent 'Dante' juu ya kiungo wa Lipuli, Shaaban Zuberi Ada katika moja ya pilika za mchezo wa leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam
    Mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Hajib akimtoka kiungo wa Lipuli, Shaaban Ada
    Kipa wa Lipuli, Agathon Mkwando akiweka mguu kuzuia shuti la kiungo wa Yanga, Raphael Daudi 

    Yanga nao walianzisha shambulizi la kasi na kufanikiwa kusawazisha baada ya kona iliyopigwa na beki wa kulia, Juma Abdul kuunganishwa nyavuni na Ngoma.
    Beki wa Lipuli Asante Kwasi alijaribu kuokolea ndani mpira huo, lakini refa Mabena hakushawishikia na beki huyo Mghana alipothubutu kumtolea maneno makali mwamuzi huyo akaonyeshwa kadi ya njano.
    Kipindi cha pili kilikuwa kigumu zaidi kwa Yanga, wachezaji wa Lipuli wakitumia mbinu ya kupoteza muda kwa kujiangusha, jambo ambalo liliwagharimu kuonyeshwa kadi tano za njano.
    Lipuli ikamalizia pungufu dakika mbili za mwisho kufuatia Kwasi kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 89 kwa kosa la kupoteza muda baada ya kujiangusha.    
    Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Youthe Rostande, Juma Abdul, Gardiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Kevin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Emmanuel Martin/Yussuf Mhilu dk71, Thabani Kamusoko, Donald Ngoma, Ibrahim Hajib na Raphael Daudi.
    Lipuli FC; Agathon Mkwando, Asante Kwasi, Samuel Mathayo, Paul Ngalema, Novaty Lufunga, Omega Seme, Seif Abdallah, Shaaban Zuberi,  Ramadhani Madebe/Jerome Lambele dk58, Malimi Busungu na Mussa Nampaka.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YAANZA NA SARE, 1-1 NA LIPULI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top