• HABARI MPYA

    Thursday, August 31, 2017

    KIDAU AITUPIA LAWAMA BODI YA LIGI KUBOMOLEWA KWA RATIBA LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAIMU Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidau ameitupia lawana Bodi ya Ligi juu ya kupanguliwa kwa ratiba Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya mechi za mzzunguko wa kwanza tu.
    Pamoja na hayo, Kidau ameunda kikosi kazi cha wataalamu wanne wa shirikisho kuangalia upya ratiba ya Ligi Kuu ili kuondoa kila aina ya kero inayoweza kuibuka katikati ya mashindano.
    Kidau ambaye ana siku tisa ofisini tangu ashike wadhifa huo, amesema kuna changamoto nyingi sana katika shirikisho, lakini kubwa ni hili ambalo wanafamilia ya mpira wa miguu wamekuwa wakijadili kwa sasa.
    Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau (kulia) ameitupia lawana Bodi ya Ligi juu ya kupanguliwa kwa ratiba ya Ligi Kuu baada ya mechi za mzunguko wa kwanza tu

    Wadau wanajadili suala la ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), kwamba baada ya michezo ya mzunguko wa kwanza tu, ratiba imetangazwa kubadilishwa. Ni kweli imebadilishwa kwa sababu ya kupisha wiki ya kalenda ya FIFA ya mechi ama za ushindani au kirafiki kati ya nchi na nchi.
    Amesema kwamba makosa yamefanywa na maofisa wa Bodi ya Ligi Kuu ambayo ndiyo yenye dhamana ya kupanga ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL); Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Ligi Daraja la Pili (SDL).
    Maofisa hao ilihali wakijua kwamba kuna wiki ya kalenda ya FIFA, walidiriki kupanga mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Sasa tuchukua nafasi hii kuomba radhi Watanzania hususani wanafamilia ya mpira wa miguu ambao kwa namna moja au nyingine wameghafirishwa na kupanguliwa ratiba.
    “Lakini suala hili haliwezi kupita hivi hivi bila hatua na kinidhamu kuchukuliwa. Rais wa TFF Bw. Wallace Karia aliniagiza nimwandikie Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu, Bw. Boniface Wambura achukue hatua za kinidhamu kwa maofisa wote waliohusika na upangaji huo wa ratiba ulioingilia ratiba ya kalenda ya wiki ya FIFA,” amesema Kidao.
    Hatua hizi za kinidhamu si kwa kupanga mechi wakati wa Wiki ya FIFA pekee, bali maofisa hao wamehusika kupanga ratiba ambayo tathmini ya uongozi imeonyesha kwamba si rafiki kwa timu zote 16 zinazoshiriki VPL.
    Hii ni kwa sababu kuna baadhi ya timu zimepangiwa kucheza mechi nyingi nyumbani au ugenini wakati wa kumaliza Ligi Kuu hasa duru la pili linaloanzia Desemba, 2017 hadi Mei, 2018.
    Ikumbukwe tu kwamba ratiba hii ilipangwa kabla ya uongozi wa Rais Wallace Karia na Kamati nzima ya Utendaji kuchaguliwa katika wadhifa huo.
    “Ninachotaka kusema  hapa ni kwamba, Kamati ya Utendaji iliyoingia madarakani Agosti 12, mwaka huu iliona upungufu na hivyo kuagizwa ratiba ipangwe upya kwa kuzingatia uwiano wa michezo ya ugenini na nyumbani ili kwa namna moja au nyingine kusiwe angalau na hisia za kupanga matokeo,” amesisitiza.
    Vita ya upangaji wa matokeo ni kubwa sana ambayo FIFA wamekuwa wakihubiri na kuagiza mashirikisho katika mabara yote kadhalika mashirikisho ya nchi kupiga vita upangwaji wa matokeo.
    Kidao amezungumza hayo baada ya kukutana na wanahabari kwa mara ya kwanza tangu kueuliwa kushika wadhifa wa Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIDAU AITUPIA LAWAMA BODI YA LIGI KUBOMOLEWA KWA RATIBA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top