• HABARI MPYA

    Tuesday, August 22, 2017

    NIYONZIMA: YANGA LAZIMA WAFE KESHO TAIFA

    Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
    KIUNGO mpya wa Simba, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima amesema kwamba kesho lazima waifunge timu yake ya zamani, Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kubeba Ngao ya Jamii. 
    Kikosi cha Wekundu wa Msimbazi Simba, leo asubuhi kimefanya mazoezi ya mwisho kabla ya kuwavaa Yanga kesho katika mchezo wa Ngao ya Jamii kuashiria ufunguzi wa pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Niyonzima alisema kwamba, tayari amekwishazoeana na wachezaji wenzake kwenye kikosi hicho na anaamini watashirikiana kuipatia ushindi timu yao kesho.
    Haruna Niyonzima amesema Yanga SC lazima wafe Uwanja wa Taifa kesho

    Alisema, wengi wanasema safu ya ushambuliaji ya Simba ni butu kutokana na kushindwa kufunga mabao, lakini anawahakikishie mashabiki na wapenzi wa timu hiyo kuwa kila mchezaji anaweza kufunga kwenye mchezo huo hata akiwa beki.
    “Nawahakikishia kila mchezaji kwenye kikosi cha Simba anaweza kufunga, ushindi lazima upatikane kwenye mchezo huo na kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu naamini kila kitu kitakwenda sawa, kwani tayari tumekwishazoeana,” alisema Niyonzima.
    Simba ambao walirejea jijini Dar es Salaam jana mchana wakitokea Unguja ambako waliweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo huo, leo asubuhi waliendelea na mazoezi yao kwenye Uwanja wa Boko Veterani uliopo Ununio, kocha wa timu hiyo, Joseph Omog aliwapa wachezaji wake mbinu za mwisho kwa ajili ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo.
    Katika mazoezi hayo, kikosi cha Simba kilionekana kufanya zoezi la mashambulizi kutokea kwa winga za pembeni na kupeleka mbele na kutawala zaidi katikati sehemu ya kiungo.
    Katika kambi yao visiwani Zanzibar, Simba ilicheza mechi mbili za kujipima nguvu ambazo ni dhidi ya Mlandege FC ambayo walitoka sare ya bila kufungana na nyingine ni dhidi ya Gulioni ambayo waliibuka na ushindi wa mabao 5-0.
    Simba na Yanga zinatarajiwa kushuka dimbani kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo wa ufunguzi wa pazia la Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 26 mwaka huu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NIYONZIMA: YANGA LAZIMA WAFE KESHO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top