• HABARI MPYA

    Wednesday, August 30, 2017

    SIMBA WAPANGA KUMFIKISHA MAHAKAMANI BUSWITA KWA UTAPELI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    UONGOZI wa klabu ya Simba ya Dar es Salaam umesema kwamba utamfungulia mashitaki kiungo Pius Buswita kwa madai ya kuwafanyia utapeli.
    Hatua hiyo inafuatia kiungo huyo aliyeng’ara na Mbao FC msimu uliopita kukiri kusaini mikataba ya klabu zote mbili kongwe nchini, Simba na Yanga msimu huu.
    Pamoja na mchezaji huyo kufungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutojihusisha na soka kwa mwaka mmoja – Simba SC haijaridhika na inataka kumchukulia hatua kali zaidi.
    Akizungumza mjini Dar es Salaam leo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Haji Manara amesema kwamba ni kweli waliingia mkataba na mchezaji huyo kama alivyokubali, lakini walishindwa kukamilisha usajili wake kutokana na mchezaji huyo kukata mawasiliano nao kabla ya kuibukia kwa mahasimu, Yanga.
    Simba imepanga kumfikisha mahakamani Pius Buswita kwa madai ya kuwatapeli

    Amesema kwa sababu hiyo watampeleka mahakamani Buswita ili arejeshe fedha za Simba alizochukua na kusaini mkataba.
    Pamoja na hayo, Manara amesema kwamba hawakuwa na shida sana na Buswita kwa sababu ndani ya kikosi chao wana viungo wengi na bora.
     “Tulikosa mawasiliano na mchezaji huyo mara baada ya kuingia naye  
    mkataba jambo ambalo lilisababisha tushindwe kupeleka jina lake TFF kutokana na kushindwa kukamilisha baadhi ya taratibu," alisema.
    Manara alisema kwa sasa wamegundua kuwa mchezaji huyo alikuwa na nia ya kuwaibia, hivyo wanafanya mpango wa kuhakikisha wanamfungulia mashitaka kwa hicho alichokifanya ili iwe fundisho kwa wengine pia.
    Wakati huo huo: Kikosi cha Simba SC kinatarajariwa kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Hadrock FC kutoka Pemba Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam Ijumaa.
    Timu hiyo inashiriki Ligi Kuu ya Zanzibar kanda ya Pemba na kocha wa Simba, Mcameroon Joseph Omog atawatumia wachezaji ambao hawajaitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars katika mchezo huo.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Haji Manara amesema kwamba lengo la mchezo huo ni kuendelea kukinoa kikosi hicho kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA WAPANGA KUMFIKISHA MAHAKAMANI BUSWITA KWA UTAPELI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top