• HABARI MPYA

    Saturday, August 26, 2017

    AZAM FC IPO KAMILI GADO KWA AJILI YA NDANDA MTWARA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAKATI kikiendelea na mazoezi ya mwisho kabla ya kuuanza msimu mpya kwa kukabiliana na Ndanda, kikosi cha Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kipo kamili kabisa kuelekea mchezo huo.
    Mchezo huo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utafanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara kesho Jumamosi kuanzia saa 10.00 jioni.
    Kikosi hicho tayari kimewasili mkoani Mtwara tokea juzi na jana kilifanya mazoezi ya kwanza mkoani humo, huku leo Ijumaa saa 10.00 jioni kikitarajia kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja huo utakaohodhi mtanange huo.
    Wachezaji wote wa Azam FC waliokuwemo kwenye msafara wa timu, wako kwenye hali nzuri na morali ya juu tayari kuanza mapambano ya kuwania taji la ligi hiyo.
    Habari njema kuelekea mchezo huo, ni kikosi hicho kutumia jezi mpya kabisa za msimu huu, ambazo watazizindua rasmi kwenye mtanange huo unaotarajiwa kuwa mkali na wa aina yake kutokana na upinzani wa pande zote mbili.
    Katika kujiandaa na msimu huu, Azam FC imecheza jumla ya mechi 10, ikishinda tano, sare tatu na kufungwa miwili huku ikifunga jumla ya mabao 16.
    Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita, ilianza kwa kupiga na mabingwa wa Rwanda, Rayon Sports na kupoteza kwa jumla ya mabao 4-2, kabla ya kutoka suluhu na Mbeya City, ikapoteza kwa kufunga 2-0 na Njombe Mji lakini ikailaza Lipuli ya Iringa mabao 4-0, mechi hizo tatu ikicheza Nyanda za Juu Kusini.
    Iliporejea jijini Dar es Salaam, ikailaza KMC bao 1-0, bao pekee likifungwa na Nahodha Msaidizi Aggrey Morris, kwa njia ya mkwaju wa penalti baada ya Wazir Junior kuangushwa ndani ya eneo la hatari.
    Baada ya mchezo huo, kikosi hicho kikaenda kumalizia mechi za majaribio nchini Uganda kwa kambi ya siku 10 na kutoka sare mabao 2-2 dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), ikatoka sare nyingine ya 1-1 na Mabingwa wa Uganda KCCA kabla ya kuzichapa URA (2-0), Onduparaka (3-0) na Vipers (1-0).
    Azam FC inaanza msimu mpya wa ligi ikiwa na baadhi ya sura mpya, ambazo ni za wachezaji vijana wenye vipaji, ambao baadhi yao wametoka kwenye kituo cha kukuza vipaji cha timu hiyo ‘Azam FC Academy’ kama vile mshambuliaji anayekuja vizuri Yahya Zayd, kiungo Bryson Raphael, Swalehe Abdallah (Majimaji), Joseph Kimwaga, kipa Benedict Haule (Mbao FC)
    Wachezaji wengine wapya walioongezwa kwenye kikosi hicho ni Mchezaji Bora Chipukizi wa msimu uliopita, Mbaraka Yusuph (Kagera Sugar), mshambuliaji Wazir Junior, beki wa kushoto Hamimu Karim (Toto Africans), Idd Kipagwile (Majimaji) na kipa Mghana Razak Abalora (WAFA FC).
    Pamoja na usajili huo, pia safari hii Azam FC imepata kibali cha Uhamisho wa Kimataifa (ITC) cha kumtumia winga wake, Enock Atta Agyei, ambaye alishindwa kutumika msimu uliopita kwenye mechi za mashindano rasmi hapa nchini baada ya kutokuwa na umri wa miaka 18 (aliotimiza Desemba mwaka jana) sambamba na kibali hicho.
    Ingizo la wachezaji hao, limeonekana kuimarisha kikosi hicho ambacho kimeonekana kufanya vizuri sana katika mechi zake za mwisho za maandalizi nchini Uganda.
    Washambuliaji wake, Yahaya Mohammed, Yahya Zayd na Wazir Junior, wameonekana kufanya vizuri kwenye maandalizi hayo katika eneo la kucheka na nyavu, hali ambayo inaleta matumaini ya kikosi hicho kunufaika na mabao msimu huu kutokana na ukali wa safu yake.
    Huku pia washambuliaji wengine Mbaraka Yusuph aliyetoka kwenye majeruhi na Shaaban Idd, anayeendelea na matibabu wakitarajiwa nao kufanya makubwa kwenye eneo hilo pale watakapokaa sawa na kuwa fiti tayari kwa ushindani.
    Kihistoria kwenye mechi za ligi timu hizo zimekuwa na upinzani mkali, ambapo Azam FC imekutana na Ndanda mara saba (sita VPL na mara moja kwenye FA Cup).
    Katika mechi hizo Azam FC imeshinda mara nne, mara tatu ikiwa kwenye ligi na mara moja kwenye robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) huku Ndanda ikishinda mara mbili na mchezo mmoja ukiisha kwa sare.
    Jumla ya mabao 15 yamefungwa kwenye mechi hizo zote (ukiwa ni wastani wa mabao mawili kila mechi), Azam FC ikiwa imefunga tisa, na Ndanda ikifunga sita.
    Mara ya mwisho msimu uliopita kwenye mchezo uliofanyika uwanja huo, Azam FC inayodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water yanayokata kiu yako, Benki ya NMB na Tradegents, ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-1, lakini ziliporudiana Azam Complex, matajitri hao walishinda 1-0 bao lililofungwa na Yahaya Mohammed kufuatia pande safi la juu la Nahodha Himid Mao ‘Ninja’.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC IPO KAMILI GADO KWA AJILI YA NDANDA MTWARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top