• HABARI MPYA

    Tuesday, August 29, 2017

    MSUVA KUJIUNGA NA STARS JUMATANO, BANDA ANATUA LEO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva, anayechezea Difaa Hassan El-Jadida ya Morocco atajiunga na kikosi cha timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars Jumatano, wakati beki Abdul Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini anawasili leo.
    Msuva ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga amtarajie Jumatano na atafurahi kujiunga na timu yake ya taifa kwa mara ya kwanza akitokea nje ya Tanzania.
    Banda naye ameondoka leo asubuhi Afrika Kusini, wakati wachezaji wengine wanaocheza nje, akiwemo Nahodha, Mbwana Samatta w KRC Genk ya Ubelgiji, Farid Mussa wa Tenerife ya Hispania, Elias Maguri wa Dhofar FC ya Oman na Orgenes Mollel wa FC Famalicao ya Ureno wamekwishawasili.   
    Simon Msuva atajiunga na kikosi cha Taifa Stars Jumatano kwa ajili ya mchezo na Botswana Jumamosi

    Taifa Stars imeanza kujifua leo asubuhi kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam baada ya wachezaji wote wanaocheza nyumbani kuwasili tayari kwa mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Botswana Jumamosi Uwanja wa Uhuru.
    Kikosi hicho kilichoweka kambi hoteli ya Sea Scape iliyoko Kunduchi, Dar es Salaam kina makipa Aishi Manula (Simba SC), Mwadini Ally (Azam FC) na Ramadhani Kabwili (Yanga SC).
    Mabeki ni Gardiel Michael (Yanga SC), Boniphas Maganga (Mbao FC), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Kelvin Yondani (Yanga SC), Salim Mbonde (Simba SC) na Erasto Nyoni (Simba SC).
    Viungo ni Himid Mao (Azam FC), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Mzamiru Yassin (Simba SC), Said Ndemla (Simba SC), Simon Msuva (Difaa El Jadidah/Morocco), Shiza Kichuya (Simba SC), Farid Mussa (CD Tenerife/Hispania) na Orgenes Mollel (FC Famalicao/Ureno).
    Washambuliaji ni Raphael Daudi (Yanga SC), Kelvin Sabato (Azam FC), Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji) na Elias Maguli (Dhofar FC/Oman).
    Benchi la Ufundi la Mayanga linaundwa na yeye mwenyewe ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUVA KUJIUNGA NA STARS JUMATANO, BANDA ANATUA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top