• HABARI MPYA

    Monday, July 17, 2017

    WACHEZAJI WOTE WA AZAM WAPIMWA AFYA CHAMAZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WACHEZAJI wote wa Azam FC pamoja na benchi la ufundi, jana wamepimwa afya makao makuu ya klabu, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, jambo ambalo ni utaratibu wake wa kawaida kila kabla ya msimu mpya.
    Zoezi hilo limeendeshwa na jopo la utabibu la klabu hiyo chini ya daktari Mwanandi Mwankemwa na Twalib Mbaraka kwa kushirikiana na Kampuni ya Afya ya Immi Life ambayo makao makuu yake yapo nchini India, iliyokuwa ikiwapima moyo wachezaji hao.
    Akizungumza jana, Daktari wa Azam FC Mwanandi Mwankemwa, alisema kuwa safari hii wameamua kutilia msisitizo kutokana na vifo vya ghafla vinavyotokea katika viwanja tofauti duniani.
    Kipa Mwadini Ali akifanyiwa vipimo vya afya jana makao makuu ya klabu, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam
    “Hawa watu wa Immi Life wanakipimo kinachoitwa ECG, ambacho kimeunganishwa kwenye mtandao na mabingwa wa moyo waliopo nchini India na wengine waliopo Uingereza, kama wachezaji wataonekana wanamatatizo wale mabingwa wa mtandao watatupa majibu mwishoni baada ya zoezi hili,” alisema.
    Alisema vipimo vingine walivyopimwa wachezaji ni katika kuangalia kama figo zao zinafanya kazi vizuri, ini, bandama, presha na sehemu zingine za tumbo au kama kuna matatizo yoyote ya uvimbe kwenye mwili.
    Naye Oparesheni Meneja wa Immi Life, Audats Mwemezi, alisema kuwa zoezi wanalofanya ni jipya kabisa hapa nchini, likiwa limedhamiria kujua hali za kiafya kwa wachezaji kabla ya kuingia viwanjani.
    “Kumekuwa na kasumba ya wachezaji kudondoka viwanjani kwa ajili ya matatizo ya moyo, hii itawapa nafasi wachezaji pamoja na madaktari wa timu za soka kujua hali ya afya ya mchezaji kama inaruhusu kuendelea na mchezo au anaweza kupata matatibabu zaidi,” alisema.
    Alisema wao kama taasisi wamefanikiwa kukusanya madaktari bingwa mbalimbali duniani na kutengeneza mfumo ambao utakuwa unaweza kuchukua kipimo na kukituma kwenye mtandao kabla ya kupata majibu ya taarifa zao za kiafya.
    “Lakini sio kwa wachezaji peke yao, hili ni zoezi tunataka lifanyike nchi nzima chini ya Wizara ya Afya tuweze kuwasaidia Watanzania kwa ujumla na wanamichezo, maana michezo kila siku tunasema inarudi chini lakini vitu vingine vinavyochangia ni afya, afya za wanamichezo huwa haziangaliwi wanamichezo wanaingia kwa ajili ya vipaji vyao lakini hatuangalii suala la afya ambalo ni muhimu sana,” alisema.
    Akiwakilisha wachezaji wenzake waliofanyiwa vipimo hivyo, mmoja wa manahodha wa Azam FC, beki kisiki Aggrey Morris, alisema kuwa jambo hilo walilofanyiwa ni kama furaha kwao ya kutambua afya zao.
    “Ni jambo zuri kwetu ukiangalia wachezaji wengi wanapata matatizo unakuta mtu kaanguka tu ghafla uwanjani kumbe inakuwa hatujapima afya zetu, kwa hiyo mimi nawasihi tu wachezaji wenzangu ni bora kupima afya ili kupata kujitambua hali yako ipo vipi kuliko kukurupuka tu kucheza bila kujua afya yako,” alisema.
    Azam FC imekuwa na utaratibu mzuri sana wa kujali afya za wachezaji, ambapo mara kadhaa imekuwa ikiwasafirisha wachezaji kwenda nchini Afrika Kusini au India, pale wanaposhindwa kupatiwa matibabu stahiki hapa nchini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WACHEZAJI WOTE WA AZAM WAPIMWA AFYA CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top