• HABARI MPYA

    Tuesday, July 18, 2017

    VIGOGO WA SOKA HISPANIA WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA RUISHWA

    RAIS wa Shirikisho la Soka Hispania, Angel Maria Villar kwa pamoja na mwanawe wa kiume na Maafisa wengine watatu wa shirikisho hilo wamekamatwa kwa uchunguzi wa tuhuma za Rushwa.
    Taarifa ya Kikosi Maalum cha Kushughulikia Rushwa nchini Hispania, maarufu kama Guardia Civil imesema kwamba Villar, mwanawe, Gorka Villar na Maafisa wengine watatu walikamatwa wakati wanajiandaa kutoka ofisi za makao makuu ya shirikisho hilo.
    Villar pia ni Makamu wa Rais mkuu wa FIFA na UEFA na Polisi imesema kwamba watu wengine watatu waliokamatwa ni pamoja na Juan Padron, Makamu wa Rais wa Masuala Uchumi na Rais na Katibu wa shirikisho la  Tenerife.
    Rais wa Shirikisho la Soka Hispania, Angel Maria Villar amekamatwa kwa tuhuma za Rushwa 

    Polisi imesema watu watano wamekamatwa kwa makosa ya kutimia vibaya madaraka yao, matumizi mabaya ya fedha, rushwa na kughushi nyaraka mbalimbali na wote wanafanyiwa uchunguzi katika operesheni maalum iliyopewa jina 'SOULE.'
    Baada ya kukamatwa kwa vigogo hao, Waziri wa Elimu, Utamaduni na Michezo wa Hispania, Inigo Mendez de Vigo alisema kupitia Televisheni ya taifa ya nchi hiyo kwamba; "Sheria za Hispania zinatimizwa, sheria ni sawa kwa wote, na hakuna mtu aliye juu ya sheria,".
    Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) nalo likasema katika taarifa yake kwamba; '"Kuhusu taarifa za Villar Llona. Hatuna cha kusema kwa sasa,".
    Villar mwenye umri wa miaka 67 sasa, amekuwa kiongozi wa soka ya Hispania tangu mwaka 1988 na mafanikio yake ni pamoja na ushindi wa timu ya taifa wa Kombe la Dunia mwaka 2010 na Kombe la Ulaya mwaka 2008 na 2012.
    Villar pia amekuwa kwenye siasa za FIFA na UEFA tangu miaka ya 1990 na amefanya kazi kwa karibu na viongozi mbalimbali wa kimataifa.
    Mtoto wake wa kiume, Gorka, miaka ya karibuni amefanya kazi katika Bodi ya Soka Amerika Kusini (CONMEBOL) kama Mkurugenzi wa Sheria kisha Mtendaji Mkuu kama Mkurugenzi Mkuu kwa Marais watatu, ambao nao walimulikwa na shirika la Upelelezi la Marekani kwa ufisadi pia. Gorka Villar aliondoka CONMEBOL Julai 2016.
    Enzi zake, Angel Maria Villar alikuwa kiungo wa Athletic Bilbao na timu ya taifa ya Hispania kabla ya kustaafu soka na kufanya kazi kama Mwasheria na kiongozi wa soka. 
    Alichaguliwa Kamati Kuu ya UEFA miaka 25 iliyopita na ya FIFA miaka 19 iliyopita. Pia amekuwa 'mtu mzito' katika Kamati za Marefa za FIFA na UEFA.
    Na baada ya mafanikio hayo, Villar akaamua kupambana na kuchukua nafasi ya Michel Platini ya Urais wa UEFA mwaka jana.
    Kabla ya kujiunga na CONMEBOL, Gorka Villar alikuwa Mwanasheria maarufu wa masuala ya kimichezo mjini Madrid. 
    Alimsaidia muendesha baiskeli, Alberto Contador kushinda Rufaa yake Mahakama ya Usuluhishi ya Kimichezo (CAS) baada ya kupatikana na hatia ya kutumia dawa za kuongeza nguvu zilizopigwa marufuku michezoni mwaka 2010 kwenye mashindano ya kuwania taji la Tour de France.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VIGOGO WA SOKA HISPANIA WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA RUISHWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top