• HABARI MPYA

  Tuesday, July 18, 2017

  TAIFA STARS KUONDOKA KESHO KUIFUATA AMAVUBI

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kitaondoka kesho Saa 4.00 asubuhi mjini Mwanza kwenda mjini Kigali, Rwanda kwa ajili ya mechi ya marudiano na wenyeji, Amavubi Raundi ya Kwanza kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), mwaka 2018 nchini Kenya.
  Baada ya sare ya 1-1 kwenye mechi ya kwanza Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Jumamosi, Stars na Amavubi zitarudiana Julai 22 Uwanja wa Amahoro, Kigali katika mchezo wa kuamua timu ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo inayohusisha wachezaji wanaocheza nchini mwao pekee.
  Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas Mapunda amesema kwamba yamefanyika mabadiliko na sasa Taifa Stars ya kocha Salum Shaaban Mayanga itaondoka Jumatano badala ya Alhamisi, ili kuwaweka sawa kisaikolojia wachezaji pamoja na hali ya utulivu wakiwa nchini Rwanda kabla ya  mchezo huo.
  Lucas amesena kikosi hicho kina majeruhi wawili tu, ambao wote mabeki wa kulia, Shomary Kapombe na Hassan Kessy ambao hata hivyo wote watasafiri na timu kesho.
  Jumamosi Stars ilianza vibaya kampeni za kuwania tiketi ya CHAN 2018 nchini Kenya, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Rwanda katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya mtoano.
  Matokeo hayo yanamaanisha Taifa Stars italazimika kwenda kushinda ugenini mjini Kigali Julai 22 ili kusonga mbele katika kuwania tiketi ya CHAN mwakani, ambako itamenyana na mshindi kati ya Sudan Kusini na Uganda zilizotoa sare ya 0-0 pia jana mjini Juba.
  Siku hiyo, Dominique Savio Nshuti alianza kuifungia Amavubi dakika ya Dk 17 akiitelezea krosi ya Emmanuel Imanishimwe kumtungua kipa bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Aishi Salum Manula anayehamia Simba SC kutoka Azam, zote za Dar es Salaam.
  Taifa Stars wakasawazisha bao hilo kupitia kwa Nahodha, Himid Mao Mkami ‘Ninja’ dakika ya 34 aliyefunga kwa penalti iliyotolewa na refa Alier Michael James kutoka Sudan Kusini, baada ya Rucogoza Aimable kuunawa mpira uliopigwa na beki Gardiel Michael dakika ya 32. Rwanda walipoteza muda kidogo kwa kumzonga refa kabla ya kutulia na kuruhusu adhabu hiyo ipigwe.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAIFA STARS KUONDOKA KESHO KUIFUATA AMAVUBI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top