• HABARI MPYA

    Monday, July 17, 2017

    SIMBA SC WATUA SALAMA ‘SAUZI’, WAANZA KUJIFUA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imewasili mjini Johannesburg, Afrika Kusini na wachezaji 12 tu kwa ajili kambi ya wiki mbili kujiandaa na msimu mpya.
    Washindi hao wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu Azam Sports Federation Cup (ASFC) wameondoka Dar es Salaam leo asubuhi kwa kambi hiyo ya wiki mbili.
    Walioondoka ni kipa Emmanuel Mseja, mabeki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yussuf Mlipili, Jamal Mwambeleko, Ally Shomari, Method Mwanjali, viungo Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, James Kotei, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim na washambuliaji Laudit Mavugo na Juma Luizio
    Kutoka kushoto, viungo Mghana James Kote, Nahodha Jonas Mkude na mkongwe Mwinyi Kazimoto 'Babu' wakati wa kuondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam
    James Kotei akiwa na Mratibu wa timu, Abbas Hussein JNIA wakati wa kuondoka

    Wachezaji wanaokosekana ni pamoja na waliokuwa mjini Mwanza na taifa ya taifa, Taifa Stars ambayo Jumamosi ililazimishwa sare ya 1-1 na Rwanda katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) mwakani nchini Kenya, michuano inayohusisha wachezaji wanaochesa nchini mwao pekee.
    Wachezaji hao watabaki kwenye kambi ya Taifa Stars hadi baada ya mchezo wa marudiano Julai 22 mjini Kigali, Rwanda na baada ya hapo ndipo watasafiri kwenda Johannesrburg kuungana na wenzao.
    Hao ni kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe, Salim Mbonde, viungo Muzamil Yassin, Said Ndemla na Shiza Kichuya na mshambuliaji John Bocco.
    Ikiwa Afrika Kusini pamoja na mazoezi makali ya kujiandaa na msimu mpya, Simba inayofundishwa na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog itacheza mechi za kujipima nguvu dhidi ya timu za Ligi Kuu nchini humo.
    Simba itarejea Dar es Salaam siku chache kabla ya Tamasha kubwa la kila Mwaka la Simba Day, lililopangwa kufanyika kama kawaida Agosti 8, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Siku hiyo Simba itatambulisha kikosi chake kamili cha msimu kabla ya kucheza mechi ya kirafiki na timu moja kutoka nje, baada ya kutwa iliyopambwa na burudani mbalimbali, ikiwemo zoezi la kuwauzia jezi mpya wapenzi na wanachama wa timu hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WATUA SALAMA ‘SAUZI’, WAANZA KUJIFUA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top