• HABARI MPYA

    Sunday, July 02, 2017

    KILA LA HERI TAIFA STARS MBELE YA WENYEJI BAFANA COSAFA LEO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    NYASI za Uwanja wa Royal Bafokeng, Rusternburg, Afrika Kusini leo zinatarajiwa kuwaka moto kwa mchezo kati ya wenyeji, Bafana Bafana na Tanzania, hiyo ikiwa Robo Fainali ya kwanza ya Kombe la COSAFA mwaka huu.
    Bafana Bafana imeanzia moja kwa moja hatua hiyo, wakati Taifa Stars imefika hapo baada ya kuongoza Kundi A katika hatua ya awali, ikitoa sare mbili, 1-1 na Mauritius na 0-0 na Angola baada ya kushinda 2-0 kwenye mchezo wa kwanza na Malawi.
    Tanzania ikaipiku Angola kwa wastani wa mabao baada ya kulingana nayo kwa pointi, huku timu nyingine katika kundi hilo, Mauritius na Malawi zote zikimaliza na pointi mbili kila moja.
    Nahodha Himid Mao akiwa na kiungo mwenzake wa Taifa Stars, winga Simon Msuva mazoezini jana
    Kocha wa Taifa Stars, Salum Mayanga japokuwa atamkosa beki wake wa kati Abdi Banda anayetumikia adhabu ya kadi za njano, lakini hana wasiwasi kwa sababu anaamini pengo hilo litazibwa.
    “Nimekuja na kikosi kipana huku, na tayari tumejiandaa kucheza mchezo huo bila Banda. Watanzania wasikate tamaa, mambo ni mazuri tu na matarajio yetu ni kufanya vizuri,”alisema Mayanga ambaye hata hivyo amekiri mchezo utakuwa mgumu kwa sababu wanacheza na wenyeji.
    Kocha wa Afrika Kusini, ambao ni mabingwa watetezi Stuart Baxter anataka kuitumia mechi hiyo kuwajaribu baadhi ya wachezaji ambao hawajawahi kupata nafasi timu ya taifa.
    Utakuwa mchezo wa kwanza Bafana Bafana kumenyana na Tanzania, wageni waalikwa kutoka Afrika Mashariki kwenye michuano hiyo ya nchi za Kusini mwa Afrika tangu mwaka 2011 kocha wa wakati huo, Pitso Mosimane alipopeleka kikosi Dar es Salaam kwa mchezo wa kirafiki na kushinda 1-0, bao pekee la Siyabonga Sangweni Mei 14 Uwanja wa Taifa.
    Kwa ujumla, timu hizo leo zinakutana kwa mara ya tatu, baada ya awali kabisa katika michuano ya CECAFA Castle Oktoba 26, mwaka 2002 na wenyeji Tanzania wakashinda kwa penalti 4-3 baada ya sare yab 0-0.
    Kikosi cha Tanzania leo kinatarajiwa kuwa; Aishi Manula, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Salim Mbonde, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni, Himid Mao, Simon Msuva, Muzamil Yassin, Elias Maguri na Shiza Kichuya.
    Katika benchi watakuwapo Benno Kakolanya, Salmin Hoza, Raphael Daudi, Thomas Ulimwengu, Mbaraka Yussuf, Stahmili Mbonde na Shabani Idd.
    Kila la heri Tanzania. Mungu ibariki Taifa Stars. Amin. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA LA HERI TAIFA STARS MBELE YA WENYEJI BAFANA COSAFA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top