• HABARI MPYA

  Sunday, July 23, 2017

  FEDHEHA HII TUNAIBEBEA WAPI?

  KAMA ilivyotarajiwa, Tanzania jana  imetolewa mapema kwenye michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayoshirikisha wachezaji wanaocheza nchini mwao pekee, baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 na wenyeji Rwanda Uwanja wa Kigali, uliopo Nyamirambo mjini Kigali.
  Nasema kama ilivyotarajiwa, kwa sababu baada ya Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza Jumamosi iliyopita, wengi walijua safari yetu katika mbio za CHAN ya mwakani Kenya ndiyo imeishia hapa.
  Na huo haukuwa unajimu, bali hesabu za kawaida za kisoka, kwamba baada ya kushindwa kushinda nyumbani mbele ya marefa wazuri kama wale wa Sudan walioongozwa na refa Alier Michael James kilichotarajiwa kufuatia ni kutolewa tu.
  Rwanda jana hawakutaka makuu, walicheza mchezo wa kujihami kulinda matokeo ya ugenini, muda mwingi wakiwa katika eneo lao kujilinda na kushambulia kwa kushitukiza.
  Na kwa mara nyingine tukaishuhudia, Taifa Stars ya kocha Salum Shaaban Mayanga ikionyesha ubutu wake katika safu ya ushambuliaji baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi.
  Mshambuliaji mkongwe John Raphael Bocco peke yake alipoteza nafasi tatu nzuri za kufunga mabao, tena zile za kumalizia tu baada ya kupelekewa pasi nzuri za uhakika.  
  Lakini kwa ujumla wachezaji wote wa mbele, Shiza Ramadhani Kichuya, Simon Happygod Msuva na Bocco walikosa mipango ya kuingiza mpira kwenye nyavu za Rwanda waliokuwa na mchezo mwingine mwepesi jana.   
  Marefa wa Uganda, Brian Nsubuga Miro aliyepuliza filimbi akisaidiwa na Ronald Katenya na Dick Okello walichezesha kwa haki leo. 
  Rwanda wanasonga mbele sasa watakutana na Uganda, iliyoitoa Sudan Kusini katika hatua ya mwisho ya mchujo kuwania tiketi ya CHAN ya mwakani nchini Kenya.
  Kuna mambo mengi ya kujilaumu kwa matokeo haya, lakini kubwa ni viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuonekana kabisa kutoitakia mema timu.
  Tumeona Taifa Stars jana ilivyocheza vizuri kwenye Uwanja mkubwa wa Nyamirambo wenye nyasi nzuri za bandia kiasi cha kuwafurahisha Watanzania na hata wakasahau kuhusu mchezo mbaya kwenye mechi ya kwanza Mwanza.
  Baada ya sare ya mechi ya kwanza Mwanza, Nahodha wa kikosi cha CHAN, Himid Mao hakusita kusema ‘ubovu’ wa eneo la kuchezea Uwanja wa CCM Kirumba ulikuwa kikwazo kwao.
  Himid Mao alisema ukweli, kwani Watanzania kwa maelfu walijionea kupitia ZBC 2 Uwanja mbovu mithili ya eneo la kulishia ng’ombe, jambo ambalo hata wageni, Rwanda walililalamikia mapema.
  Na suala la ubovu wa Uwanja wa Kirumba, lilionekana mapema tu Machi mwaka huu wakati ule klabu ya Yanga inataka kuutumia kwa mechi za michuano ya klabu Afrika, wakaguzi wa CAF (Shirikisho la Soka Afrika) waliagiza marekebisho yafanyike kwanza.
  Ajabu Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi alikuwa pamoja na wakaguzi hao Mwanza na akaliona hilo – lakini ameruhusu mechi ya Stars ichezwe hapo hapo.
  Ikumbukwe awali ya hapo, Taifa Stars ililazimishwa sare ya 1-1 tena na Lesotho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa Kundi L kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 Cameroon.
  Nahodha Mkuu wa Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji alizungumza baada ya mechi na akasema udogo wa eneo la kuchezea katika Uwanja wa Azam Complex, ulisababisha washindwe kushinda.
  Alisema wamezoea kucheza kwenye Uwanja mkubwa wa Taifa, ambao wakati wa mchezo huo ulikuwa umefungwa kwa ukarabati kuelekea mchezo wa kirafiki kati ya Everton na Gor Mahia ya Kenya uliochezwa Julai 13.
  Na Mkurugenzi huyo huyo wa Ufundi, Madadi ndiye aliyeruhusu mchezo dhidi ya Lesotho uchezwe Chamazi – lakini ajabu pia hata benchi la Ufundi la Taifa Stars halina sauti.
  Timu imetoka kucheza kwenye viwanja vizuri Afrika Kusini, imecheza mpira mzuri na kupata matokeo ya kuridhisha kiasi cha kuanza kuamsha hisia za wapenda soka wa Tanzania kwa timu yao.
  Lakini baada ya kurejea nyumbani, wananchi wanaanza kukatishwa tena tamaa kutokana na uzembe wa watu wale wale kila siku, tena ambao eti wanaomba tena dhamana ya kuendelea kuongoza soka ya nchi hii.
  Ni aibu kubwa kwa Taifa. Dunia iliyoshuhudia Everton wakimenyana na Gor Mahia katika Uwanja mzuri wa Tanzania siku mbili baadaye inaona timu yetu ya taifa inacheza kwenye Uwanja wenye makorongo. Fedheha iliyoje! 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: FEDHEHA HII TUNAIBEBEA WAPI? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top