• HABARI MPYA

    Saturday, July 22, 2017

    AZAM FC NA MBEYA CTY HAKUNA MBABE, SARE 0-0 SOKOINE

    Na Mwandishi Wetu, MBEYA
    TIMU ya Azam FC leo imetoka suluhu na Mbeya City jioni hii katika mchezo wake wa kwanza wa maandalizi ya msimu ujao uliofanyika Uwanja wa Sokoine mjini hapa.
    Tayari imeshajulikana kuwa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utaanza Agosti 26 mwaka huu kwa mechi mbalimbali za ufunguzi kupigwa huku Azam FC ikitarajia kuanzia ugenini siku hiyo kwa kukipiga na Ndanda katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona.
    Mbeya City ambayo iliutumia mchezo huo kutambulisha jezi zake, kabla ya kuanza mtanange iliipa tuzo maalumu Azam FC, mipira na glovu za makipa kama sehemu ya akhante baada ya kukubali mualiko wao wa kucheza mechi hiyo maalumu ya kirafiki.
    Katika mchezo huo ilishuhudiwa Azam FC ikianza kuwatumia rasmi wachezaji wake wapya, mshambuliaji Wazir Junior na kipa Benedict Haule, walioanza kucheza kwa mara ya kwanza tokea wajiunge na timu hiyo.
    Mchezo huo uliokuwa mkali na wa upinzani kwa pande zote mbili, ilishuhudiwa Azam FC ikipoteza takribani nafasi nne za wazi kupitia kwa wachezaji wake Junior, Masoud Abdallah, Yahaya Mohammed.
    Iliwachukua Azam FC dakika 29 kuweza kutengeneza nafasi nzuri ya kujipatia bao, baada ya Yahaya kuwazidi maarifa mabeki wa Mbeya City na kupiga pasi safi iliyomkuta Junior, ambaye alipiga shuti lililogonga mwamba wa pembeni kabla ya kudakwa na kipa.
    Nafasi kama hiyo ilimkuta tena, kiungo Masoud dakika ya 75, aliyeshindwa kuitumia vema krosi safi ya Yahya Zayd, baada ya kupiga shuti ambalo nalo liligonga mwamba wa juu na kutoka nje.
    Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka mjini Mbeya kesho asubuhi kuelekea mjini Makambako, Njombe kucheza na Njombe Mji, katika mechi nyingine ya kirafiki itakayofanyika Uwanja wa Makambako Julai 24 mwaka huu.
    Azam FC itahitimisha ziara ya Nyanda za Juu Kusini kwa kukipiga na Lipuli ya Iringa Julai 26 mwaka huu, katika Uwanja wa Samora.
    Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Benedict Haule, David Mwantika/Saleh dk 73, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Frank Domayo/Mudathir Yahya dk 78, Bryson Raphael/Masoud Abdallah dk 67, Salum Abubakar, Yahaya Mohammed/Idd Kipagwile dk 88, Wazir Junior/Yahya Zayd dk 61, Enock Atta/Joseph Kimwaga dk dk 67
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC NA MBEYA CTY HAKUNA MBABE, SARE 0-0 SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top