• HABARI MPYA

  Monday, July 03, 2017

  BOCCO ATUA AFRIKA KUSINI KUCHUKUA NAFASI YA MBARAKA TAIFA STARS

  Na Mwandishi Wetu, RUSTERNBURG
  MSHAMBULIAJI mpya wa Simba, John Raphael Bocco ameongezwa katika kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichopo Afrika Kusini kwenye michuano ya COSAFA Castle.
  Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Bocco aliondoka jana kwenda Afrika Kusini kuchukua nafasi ya mshambuliaji mpya wa Azam FC, Mbaraka Yussuf Abeid ambaye ni mgonjwa.
  “Mbaraka amepata matatizo kule Afrika Kusini, hali ya hewa ya baridi imemletea matatizo ambayo kwa sasa yanamzuia kucheza. Hivyo wakati tunatazama hali yake, tumemuita Bocco kwanza kuchukua nafasi,”amesema Madadi.

  John Bocco ameongezwa katika kikosi cha Taifa Stars kilichopo Afrika Kusini kwenye michuano ya COSAFA Castle

  Madadi amesema Bocco ameitwa kwa ajili ya mechi ya kwanza ya kufuzu Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) dhidi ya Rwanda Julai 14 mjini Mwanza, kwa kuwa kwa sasa hataweza kuingizwa kwenye COSAFA.
  Taifa Stars jana ilifanikiwa kwenda Nusu Fainali ya COSAFA ikiwatoa wenyeji, Bafana Bafana kwa kuwafunga 1-0, bao pekee la Elias Maguri Uwanja wa Royal Bafokeng, Rusternburg.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Olivio Saimone wa Msumbiji aliyesaidiwa na Matheus Kanyanga wa Namibia na Jackson Pavaza wa Namibia, Maguri alifunga bao hilo dakika ya 10 kwa shuti la mahesabu baada ya pasi ndefu ya kiungo Muzamil Yassin, Stars ikitoka kushambuliwa.
  Tanzania sasa itamenyana na Zambia Jumatano katika Nusu Fainali, wakati Afrika Kusini wanaangukia kwenye michuano ya Plate, inayohusisha timu zilizotolewa hatua ya Robo Fainali.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BOCCO ATUA AFRIKA KUSINI KUCHUKUA NAFASI YA MBARAKA TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top