• HABARI MPYA

    Monday, August 15, 2016

    YANGA KUWAKOSA CHIRWA, YONDAN, JUMA ABDUL MECHI YA NGAO NA AZAM JUMATANO

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    YANGA SC itawakosa wachezaji wake nyota watano katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Hao ni kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ anayesumbuliwa na maumivu ya kifundo mguu, mabeki Juma Abdul, Andrew Vincent ‘Dante’ wanaosumbuliwa na maumivu ya miguu, Kevin Yondani anayeumwa jicho na kiungo Obrey Chirwa anayeumwa goti.
    Kikosi cha kimeendelea na mazoezi leo Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa Ngao dhidi ya Azam Jumatano, kuashiria kupenuliwa kwa pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Obrey Chirwa atakosekana kwenye mchezo na Azam FC Jumatano
    Faraja zaidi ni kwamba mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma aliyekuwa majeruhi na akakosa mchezo wa kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar amerejea uwanjani.
    Ngoma leo amefanya mazoezi kikamilifu Gymkhana kuashiria kwamba anaweza kucheza dhidi ya Azam FC keshokutwa.
    Tayari Yanga imetupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kufuatia wenyeji Medeama SC kushinda 3-2 dhidi ya TP Mazembe ya DRC jana katika mchezo wa Kundi A Uwanja wa Essipong Sports mjini Takoradi, Ghana.
    Kwa matokeo hayo, Medeama watakwenda Algeria kupigania sare kwenye mchezo wa mwisho na wenyeji Mouloudia Olympique Bejaia Agosti 23 ili kwenda Nusu Fainali, siku ambayo Yanga itakuwa ikikamilisha ratiba na TP Mazembe mjini Lubumbashi. 
    Mazembe inaendelea kuongoza Kundi A kwa pointi zake 10 baada ya mechi tano, ikishinda tatu, kufungwa moja leo na sare moja, ikifuatiwa na Medeama yenye point inane, Bejaia pointi tano na Yanga inashika mkia kwa pointi zake nne. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA KUWAKOSA CHIRWA, YONDAN, JUMA ABDUL MECHI YA NGAO NA AZAM JUMATANO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top