• HABARI MPYA

  Wednesday, August 17, 2016

  KAMA YANGA WAMEFIKIA KUMUABUDU BINADAMU, BASI HATARI!

  WIKI hii imeanza kwa vitimbi katika klabu kongwe nchini, Yanga kufuatia kuvuja kwa habari za Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji kutaka kujiuzulu baada ya kile kilichodaiwa kukerwa na maneno ya Mzee wa klabu hiyo, Ibrahim Akilimali.
  Akilimali alizungumza kwenye vyombo vya Habari akisema kwamba Manji alikurupuka kwenda kuomba kwenye Mkutano wa wanachama kuikodisha klabu kwa miaka 10 bila kushauriana na wazee.
  Sikuona baya katika maelezo ya Akilimali, alisema Manji alikwenda mkutanoni wiki iliyopita kuomba kuikodisha klabu bila kujadiliana na Wazee.

  Na ukizingatia siku zote Manji katika harakari zake amekuwa akiwatumia Wazee hao hao wakiongozwa na Akilimali. Hata kwenye vita zake binafsi na mfanyabiahsara mwenzake, Reginald Mengi, Manji amekuwa akiwatumia akina Akilimali – hivyo hadi sasa sioni baya alilozungumza mzee huyo.
  Ninachoweza kuhisi, Manji na Akilamali ni marafiki waliohitilafiana labda na sasa wanakwaruzana na hii si mara ya kwanza baina yao, iliwahi kutokea wakamalizana – natarajia hata sasa watayamaliza tu.
  Watayamaliza kwa sababu Manji anamuhitaji sana Mzee Akilimali mbele ya safari.
  Jambo moja lililonisikitisha ni namna wanachama na wapenzi wa Yanga walivyozipokea habari za Manji kutaka kujiuzulu kwa masikitiko makubwa.
  Sahau kuhusu yale maigizo ya watu waliopangwa kuandamana hadi makao makuu ya klabu – lakini ukweli ni kwamba habari za Manji kutaka kuondoka Yanga ziliwashitua wapenzi wengi wa timu hiyo.
  Walizipokea kama ni kifo cha klabu yao na wakasahau kwamba, mtu huyo aliingia katika klabu hiyo mwaka 2006 kama mfadhili kwanza na baadaye kama Mwenyekiti mwaka 2012 wakati Yanga ipo tangu mwaka 1935.
  Na wakasahau kwamba huyo ni binadamu tu ambaye iko siku ataondoka kama walivyoondoka wafadhili waliomtangulia akina Abbas Gulamali, Mohamed Virani (sasa marehemu) na wengine.
  Yanga inahitaji kuendelea kuwapo kama ambavyo imeendelea kuwapo hata baada ya kuondoka kwa watu muhimu katika historia ya klabu hiyo, akiwemo Abeid Amaan Karume, rais wa kwanza wa Zanzibar ambaye ndiye aliyewajengeea jengo la makao makuu pale Jangwani.
  Lakini kwa hali ilivyo sasa ukweli ni kwamba, Yanga itayumba sana baada ya kuachwa na Manji kwa sababu tu imekosa viongozi shupavu, weledi wenye dira na wafanisi.
  Manji ndiye Mwenyekiti wa Yanga, ambaye anaongoza klabu Kidikteta kiasi kwamba, Makamu wake, Clement Sanga yupo tu kama ‘kivuli’ yeye ni ‘ndiyo mzee’ kwa lolote la Manji.
  Sanga amejisahau kwamba Manji ni kiongozi mwenzake na imefikia anamuona kama bosi wake. Hawezi kumuambia kitu, iwe anamuogopa au vipi, basi hata kumshauri nayo inashindikana!  
  Akiwa Mfadhili, Manji alitofautiana na Wenyeviti wote wa Yanga ambao aliwaweka mwenyewe madarakani, kuanzia Wakili Imani Madega na baadaye Lloyd Nchunga.
  Na kuna viongozi aliingia nao madarakani awali mwaka 2012 kama Aaron Nyanda, mchezaji wa zamani wa klabu, sasa hawapo kwa sababu hao hawakukubali kuburuzwa.
  Na wiki iliyopita ametoka kuwafukuza viongozi watatu, Ayoub Nyenzi, Salum Mkemi na Hashim Abdallah kwa sababu pia hao hawakutaka kuwa kama Sanga na wengine ambao Manji amekuwa akiwaburuza atakavyo.  
  Manji anajisahau kwamba amepewa dhamana ya kuongoza Yanga pamoja na viongozi wengine, ambao anapaswa kushirikiana nao.
  Lakini akitokea mtu wa kupingana naye tu, anaondolewa. Anafukuzwa. Makatibu wote Wakuu waliowahi kufanya kazi Yanga walifukuzwa kwa kashfa kuanzia Lawrence Mwalusako, mchezaji wa zamani wa klabu, Selestine Mwesigwa, Beno Njovu na Dk Jonas Tiboroha.
  Manji anataka anachotaka ndiyo kiwe, hataki ushauri, yeye amekuwa nani, Mungu?
  Na inasikitisha wana Yanga wa siku hizi wamekuwa legelege mno, zamani hakutokea mtu wa kuichezea Yanga kama afanyavyo Manji sasa, kwa sababu wana Yanga wa wakati huo hawakuwa watu wa kuyumbishwa.
  Walikuwa tayari kuchangia klabu yao hata kwa kutembeza bakuli, ili iende lakini si kunyanyaswa na kuyumbishwa na mtu kwa fedha zake. Hiyo siyo asili ya Yanga.
  Mmoja kati ya Wenyeviti shupavu kuwahi kutokea Yanga, aliwahi kusema; “Sitokuwa tayari kuiona Yanga ikiuzwa na kutawaliwa na mtu mmoja kwa nguvu ya pesa, masikini na mwanawe, tajiri na mali zake, Manji baki na mali zako au heshimu Katiba. Vinginevyo baki na mali zako au fadhili timu nyingine. Wazee na wanachama wachache waroho wa Yanga kuweni macho na msiwasaliti wazee wenzenu ambao walifanya juhudi kuifanya Yanga iwe na jina kubwa, mkiendelea kufanya hivyo kwa hakika historia itawahukumu, uongozi uko imara kutetea maslahi ya Yanga,”. 
  Madega alitoa kauli hii Oktoba 11, mwaka 2007, mwaka mmoja tu baada ya Manji kuanza kuifadhili Yanga kutokana na wazee na wanachama wa klabu hiyo kumuunga mkono Manji katika mgogoro wake na Madega.
  Hakuna anayeweza kushindana na Manji pale Yanga, kwa sababu ya imani tu iliyopo kwamba bila yeye klabu haiwezi kwenda.
  Na wanaoamini hivyo wengi wao ni wanachama wa kadi mpya vijana wa umri wa chini ya miaka 25 ambao bahati mbaya hawaijui vyema klabu. Wao Yanga oyee tu na Manji ndiyo mpango mzima.
  Siku zote Manji amekuwa akitengeneza mazingira ya yeye tu kuonekana mtu muhimu katika klabu, tena wakati mwingine ikidaiwa anawazuia watu wengine kusaidia klabu.
  Wakati fulani aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu, Abeid Abeid alitaka kukarabati Uwanja wa Kaunda katika kiwango kizuri cha kutumika kwa mazoezi, lakini inadaiwa Manji alizuia zoezi hilo. 
  Je, watu wanajua nyuma ya kuburuzwa na kukimbizwa kwa uchaguzi wa Yanga kulikuwa kuna nini?
  Inasemekana kuna bilionea mmoja mwenye asili ya Kiarabu alitaka kugombea na inadaiwa baada ya Manji kugundua, akaamua kuupeleka haraka uchaguzi.
  Kila siku anaharibu mahusiano ya klabu na wadau na taasisi nyingine zinazosaidia kifedha mfano TBL, Azam TV na imefikia sasa klabu haina chanzo chochote kingine cha fedha zaidi ya kumtegemea yeye.
  Na wakati haya yote yanatokea unaambiwa eti Yanga ina Kamati ya Utendaji na Makamu Mwenyekiti ni Clement Sanga. Aibu.
  Yanga ya sasa haina msingi wowote, jengo lile la makao makuu linachakaa kila kukicha, Uwanja wa Kaunda ndiyo sasa hautazamiki kabisa na Manji akiondoka tu ni kilio.
  Ndiyo maana leo ninawaambia wana Yanga umefika wakati wa kujitafakari upya na kuutafakari upya mustakabali wa klabu yao chini ya Manji. Yanga inakwenda wapi kama imefikia kumuabudu binadamu kama Mungu, basi hatari!
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAMA YANGA WAMEFIKIA KUMUABUDU BINADAMU, BASI HATARI! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top