• HABARI MPYA

    Friday, August 05, 2016

    HASIRA ZA AVEVA BAADA YA KUTOKA LUPANGO… AWASAINISA WAGENI WATANO SIMBA SC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIKU moja baada ya kuachiwa kwa dhamana, Rais wa Simba Sc Evans Elieza Aveva jioni ya leo amewasainisha mikataba wachezaji watano wa kigeni.
    Aveva alishikiliwa na Polisi, kituo kidogo cha Mabatini, Kijitonyama, Dar es Salaam kuanzia juzi hadi jana kwa tuhuma za kuhamishia fedha za klabu katika akaunti yake binafsi.
    Baada ya kuachiwa, Aveva leo amewasainisha mabeki Janvier Besala Bokungu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Method Mwanjali kutoka Zimbabwe, kiungo Mussa Ndusha kutoka DRC pia na washambuliaji Frederick Blagnon kutoka Ivory Coast na Laudit Mavugo wa Burundi.
    Watano hao wanakamilisha idadi ya wachezaji saba wa kigeni Simba SC kwa mujibu wa kanuni, wakiungana na kipa Vincent Angban raia wa ivory Coast pia na beki Juuko Murshid raia wa Uganda.
    Aveva akimkabidhi jezi Mavugo baada ya kusaini Mkataba
    Mavugo akisaini Mkataba pembeni ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Collin Frisch
    Angban na Juuko ndiyo pekee waliobaki kutoka kikosi cha Simba SC msimu uliopita katika wachezaji wa kigeni, baada ya kuachwa kwa Mrundi Emery Nimubona, Mzimbabwe Justice Majabvi na Mganda Hamisi Kiiza.
    Simba SC ilihamishia kambi yake hoteli ya Ndege Beach, Dar es Salaam jana kutoka Chuo cha Biblia mjini Morogoro kwa ajili ya kuazimisha wiki ya Simba kuelekea kielele cha sherehe za miaka 80 ya klabu, maarufu kama Simba Day Jumatatu ijayo.
    Na Simba SC imekuja mjini siku moja baada ya kufungwa 1-0 na KMC ya Kinondoni jioni ya Jumatano katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Highlands, Bigwa mkoani Morogoro.
    Huo ulikuwa mchezo wa kwanza Simba SC kupoteza chini ya kocha mpya, Mcameroon, Joseph Marius Omog baada ya awali kushinda mechi zote tatu, 5-0 dhidi ya Burkina Fasso, 2-0 dhidi ya Moro Kids na 6-0 dhidi ya Polisi Morogoro.
    Katika kilele cha sherehe za Simba Day, Wekundu wa hao Msimbazi watamenyana na AFC Leopards ya Kenya iliyochukua nafasi ya Interclube ya Angola ambayo imejitoa dakika za mwishoni.
    Aveva alihojiwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) jana na leo juu ya kuhamisha zaidi ya dola za Kimarekani 300,000 kutoka akaunti ya klabu kwenda akaunti yake binafsi.
    Fedha ambazo Aveva anadaiwa kuhamisha ni zilizolipwa na Etoile du Sahel ya Tunisia, dola za Kimarekani 300,000 zaidi ya Sh. Milioni 600 za Tanzania.
    Awali, Etoile walikuwa wazito kulipa fedha hizo kwa sababu walidumu na Okwi kwa miezi sita kabla ya kushindwana na kushitakiana hadi FIFA.
    Etoile ilimtuhumu Okwi kuchelewa kurejea klabuni baada ya kuruhusiwa kwenda kuchezea timu yake ya taifa, wakati mchezaji akadai kutolipwa mishahara kwa zaidi ya miezi mitatu. 
    Aveva amkimkabidhi jezi Said Ndusha baada ya kusaini Mkataba
    Janvier Bokungu akisaini Mkataba pembeni ya Frisch
    Aveva akimkabidhi jezi Blagnon baada ya kusaini Mkataba
    Blagon akisaini Mkataba na Frisch
    Aveva akimkabidhi Bokungu jezi
    Aveva akimkabidhi Mwanjali jezi
    Mwanjali (katikati) akisaini huku akielekezwa na Frisch. Kushoto Aveva anashuhudia

    Mwishowe Okwi aliruhusiwa na FIFA kutafuta klabu ya kuchezea wakati kesi yake na Etoile inaendelea – naye akarejea klabu yake ya zamani, SC Villa ya Uganda, ambayo baadaye ilimuuza Yanga SC mwaka 2014.
    Baada ya nusu msimu, Okwi akavurugana pia na Yanga hadi kufikishana TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) ambako aliruhusiwa kuondoka bure Jangwani, hivyo kujiunga tena na Simba SC kama mchezaji huru.
    Simba SC ikamuuza tena Okwi kwa dola za Kimarekani 100,000 klabu ya SonderjyskE ya Ligi Kuu ya Denmark, ambako anakoendelea na kazi hadi sasa. 
    Desemba mwaka jana, FIFA iliipa Etoile siku 60 kuwa imekwishalipa dola 300,000 za Simba SC, vinginevyo watachukuliwa hatua kali, ikiwemo kufungiwa kucheza mashindano yoyote. 
    Mkuu wa Idara ya Uchunguzi wa Sekta ya Uma ya TAKUKURU, Leonard Mtalai alisema baada ya fedha hizo kuhamishiwa kwenye akaunti ya Aveva, dola 62,000 zilitumwa Hong Kong, China.
    Mtalai alisema kwa sasa TAKUKURU inashirikiana na Taasisi ya Rushwa ya China kuchunguza ili kujua fedha zilizotumwa Hong Kong zilitumikaje.
    Pamoja na Aveva, Wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC walihojiwa jana na leo na TAKUKURU.
    Na inadaiwa Maofisa wa TAKUKURU walikwenda kufanya ukaguzi ofisini kwa Aveva pia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HASIRA ZA AVEVA BAADA YA KUTOKA LUPANGO… AWASAINISA WAGENI WATANO SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top