• HABARI MPYA

    Tuesday, May 10, 2016

    SIMBA YAWAPOZA ‘MAPROO’ WAKE, WAWILI WAKUBALI KUIFUATA TIMU SONGEA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WACHEZAJI wawili wa Simba kati ya saba waliogoma kusafiri na timu jana kwenda Songea mkoani Ruvuma kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Majimaji kesho wameondoka leo.
    Hao ni kipa Vincent Angban raia wa Ivory Coast na kiungo Mzimbabwe Justice Majabvi ambao wameondoka na basi leo asubuhi.
    Wawili hao wameondoka baada ya kikao cha pamoja baina ya wote waliogoma na Rais wa klabu, Evans Aveva kilichofanyika jana mjini Dar es Salaam.
    Kiungo Mzimbabwe, Justice Majabvi amekwenda Songea leo asubuhi kuiongezea nguvu Simba

    Wachezaji hao waligoma kwa sababu ya kucheleweshewa mishahara ya Aprili na uongozi wa Simba ulisema jana mishahara imechelewa kwa sababu wadhamini, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) hawajatoa fedha.
    Habari zisizo za uhakika zinasema Rais Aveva jana aliwalipa wachezaji hao waliogoma na kuwateua wawili kati yao, Angban na Majabvi kwenda kuiongezea nguvu timu Songea.  
    Wengine waliogoma ni beki Mrundi Emery Nimubona, kiungo mzawa Mwinyi Kazimoto, Waganda beki Juuko Murshid, kiungo Brian Majwegga na mshambuliaji Hamisi Kiiza.
    Mbali na hao waliogoma Simba kesho itawakosa pia viungo Jonas Mkude, Awadhi Juma na washambuliaji Ibrahim Hajib na Raphael Kiongera, ambao nao hawajasafiri na timu kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuwa majeruhi na kutumikia adhabu za kadi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAWAPOZA ‘MAPROO’ WAKE, WAWILI WAKUBALI KUIFUATA TIMU SONGEA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top