• HABARI MPYA

    Sunday, May 22, 2016

    JUMA ABDUL JAFFAR MNYAMANI MCHEZAJI BORA LIGI KUU APRILI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BEKI wa kulia, Juma Abdul Jaffar Mnyamani ameteuliwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mwezi Aprili, 2016 baada ya kuwashinda kwa kura mshambuliaji Mzimbabwe Donald Ngoma anayecheza naye Yanga SC ya Dar es Salaam na kiungo Hassan Dilunga wa JKT Ruvu ya Pwani.
    Katika rekodi za Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) iliyoketi Jumamosi Iliyopita, imeonesha kwamba Abdul alicheza mechi zote tano za Ligi Kuu kwa mwezi Aprili ambapo pia aliifungia timu yake bao katika harakati za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2015/16.
    Juma Abdul Jaffar Mnyamani (kushoto) ndiye mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwezi Aprili  
    Rekodi hizo pia zinaonyesha kwamba beki huyo hakuonyeshwa kadi hata moja katika michezo hiyo mitano sambamba na kutoa mchango mkubwa katika michezo aliyoshiriki kwa mwezi Aprili, 2016. Abdul atazawadiwa fedha Sh. 1,000,000 (milioni moja) na wadhamini wa Ligi hiyo, Kampuni ya mahiri ya simu za mkononi ya Vodacom.
    Uwezo aliouonyesha Abdul ulisababisha Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ kumjumuisha katika kikosi chake kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya Harambee Stars ya Kenya kadhalika Mapharao wa Misri katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Juni 4, mwaka huu.
    Wachezaji bora wa miezi minne iliyopita ni kiungo Thaban Kamusoko wa Yanga SC (Desemba 2015), beki Shomari Kapombe wa Azam (Januari 2016), Mshambuliaji Mohamed Mkopi wa Tanzania Prisons (Februari 2016) na Shiza Ramadhani Kichuya wa Mtibwa Sugar (Machi 2016).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JUMA ABDUL JAFFAR MNYAMANI MCHEZAJI BORA LIGI KUU APRILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top