• HABARI MPYA

    Thursday, May 26, 2016

    TAIFA STARS YAIFUATA HARAMBEE BILA SAMATTA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta (pichani kushoto) hataweza kusafiri na Taifa Stars kwenda Nairobi, Kenya kucheza na wenyeji Harambee Stars mchezo wa kirafiki wa kimataifa.
    KRC Genk imemuombea Samatta kutorejea nchini kwa ajili ya mchezo huo kwa sababu inamuhitaji katika mechi ya mchujo wa mwisho wa kuwania tiketi ya kucheza michuano ya Europa League.
    Na kwa ombi hilo la timu hiyo ya Ubelgiji, Samatta hatakuwemo kwenye msafara wa unaoondoka kesho saa 12.00 Alfajiri chini ya makocha wake, Charles Boniface Mkwasa na Hemed Morocco.
    Mchezo huo ni maandalizi ya kujiandaa kucheza Misri Juni 4, 2016 katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON-2017) wakati Kenya pia itakuwa na mchezo dhidi ya Congo.
    Mkwasa maarufu kama Master, alitangaza kikosi cha timu hiyo leo Mei 18, 2016 mbele ya waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa mikutano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.

    Mchezo huo unadumisha uhusiano na upendo wa enzi wa nchi za Kenya na Tanzania na umeingizwa kwenye orodha ya viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
    Kikosi cha Stars kina makipa, Deogratius Munishi (Young Africans), Aishi Manula (Azam FC) na Benny Kakolanya (Tanzania Prisons) wakati mabeki ni Mwinyi Haji na Juma Abdul (Young Africans), Aggrey Moris, David Mwantika na Erasto Nyoni (Azam FC), Mohammed Hussein (Simba) na Vicent Andrew (Mtibwa Sugar).
    Viungo ni Himid Mao, Farid Mussa (Azam), Jonas Mkude na Mwinyi Kazimoto (Simba), Mohammed Ibrahim na Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar), Ismail Issa (JKT Ruvu), Juma Mahadhi (Coastal Union) na Hassan Kabunda (Mwadui FC) wakati washambuliaji ni Thomas Ulimwengu (TP Mazembe), Mbwana Samatta (KDC Genk), Elias Maguli (Stand United), Ibrahim Ajib (Simba), John Bocco (Azam), Deus Kaseke (Young Africans) na Jeremiah Juma (Tanzania Prisons).
    Wakati huo huo: Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), limemteua Michael Richard Wambura kuwa Kamishna wa mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Rwanda na Msumbiji unaotarajiwa kufanyika jijini Kigali, Juni 3, 2016.
    Wambura ambaye amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), atakuwa Balozi mzuri katika mchezo huo unaokutanisha timu ambazo nchi imepana nazo. Msumbiji iko Kusini mwa Tanzania wakati Rwanda iko Magharibi mwa Tanzania.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS YAIFUATA HARAMBEE BILA SAMATTA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top