• HABARI MPYA

    Wednesday, May 25, 2016

    BILA KUWEKA FEDHA KWENYE TIMU, SIMBA WATASUBIRI SANA!

    KWA mara nyingine tena, mwakani Simba SC haitashiriki michuano ya Afrika, baada ya kuzidiwa kete na wapinzani, Azam na Yanga katika mbio za mataji nchini. 
    Katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba imemaliza nafasi ya tatu nyuma ya Azam waliomaliza nafasi ya pili na Yanga SC walioibuka mabingwa.
    Yanga kwa kuwa bingwa, itacheza tena michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
    Na katika Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Simba walitolewa katika Robo Fainali na Coastal Union ya Tanga ambayo imeshuka daraja kutoka Ligi Kuu.
    Fainali ya Kombe la TFF, maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) inafanyika leo ikizikutanisha Azam na Yanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

    Tayari TFF imekwishaitangaza Azam FC  itacheza Kombe la Shirikisho mwakani, kwa kuwa Yanga tayari wana tiketi ya Ligi ya Mabingwa, hivyo fainali ya leo ya Kombe la ASFC itatuhitimishia msimu na kupata fursa ya kujua mbabe baina ya timu hizo.
    Mara ya mwisho Simba SC ilicheza michuano ya klabu Afrika mwaka 2013, baada ya kuwa bingwa wa Ligi Kuu mwaka 2012, msimu ambao iliwafunga mahasimu, Yanga mabao 5-0.
    Lakini baada ya msimu wa 2012, Simba ikaanza kuvuruga kikosi chake na wachezaji nyota wakaanza kuondoka mfululizo.
    Haikuwa ajabu katika Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2013 Simba ikatolewa Raundi ya Kwanza tu, tena ikifungwa nyumbani na ugenini na Recreativo de Lobolo ya Angola.
    Ilifungwa 1-0 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 4-0 Angola. 
    Tangu hapo, Simba imekuwa ‘rojorojo’ katika mashindano ya nyumbani na kushindwa kupata tena nafasi ya kucheza michuano ya Afrika.
    Visingizio, malalamiko na sababu nyingi ndivyo vimekuwa vikifuatiwa kutoka kwa viongozi wa Simba kila baada ya msimu.
    Wiki iliyopita, Rais wa Simba SC, Evans Aveva aliitisha mkutano na Waandishi wa Habari akaeleza sababu nyingi, akalaumu wachezaji na TFF.
    Lakini sababu zilizoonekana kuwa za msingi kabisa ni kusema ushindani katika Ligi Kuu umeongezeka hususan baada ya ujio wa timu imara ya Azam.
    Ni kweli, kabla ya Azam, Simba na Yanga zilikuwa zinapokezana nafasi mbili za juu katika Ligi Kuu, lakini ujio wa timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake umefuta desturi hiyo.
    Simba sasa imeyumba mno, kwa sababu inazidiwa kiuchumi na Azam na Yanga, ambayo mbali na udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), inajivunia pia Mwenyekiti wake, milionea Yussuf Manji ambaye anaweka fedha nyingi katika timu.
    Aina ya wachezaji wanaosajiliwa Azam na Yanga ni tofauti kabisa na wale ambao wanasajiliwa na Simba SC hivi sasa.
    Na mbaya zaidi, Simba hata inapobahatisha wachezaji wazuri kuishi nao imekuwa taabu pia – kwa sababu hawako vizuri kiuchumi.
    Mwishoni mwa msimu kimeshuhudiwa kituko cha wachezaji wa kigeni kugoma kwa sababu ya kucheleweshewa mishahara.
    Na kilichofuata baada ya hapo, si kuketi nao chini kumaliza tofauti, bali imeelezwa wameachwa.
    Maana yake sasa msimu ujao Simba itaanza kujiumba upya kwa kutafuta wachezaji wa kuziba nafasi za wageni wanaoondoka. 
    Jana Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amekaririwa akisema kwamba wachezaji 33 wamependekezwa na Kamati ya Ufundi wasajiliwe kwa ajili ya msimu ujao.
    Poppe, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), alisema kwamba orodha hiyo itawasilishwa Kamati ya Usajili na kujadiliwa ili kupata orodha fupi ya wachezaji wa kusajiliwa.
    Hata hivyo, Poppe alisema kwamba kabla ya mchakato huo, jana jioni walitarajiwa kukutana na kocha Mganda, Jackson Mayanja kupokea ripoti yake pia.
    Alisema Mayanja naye atakuwa na orodha ya wachezaji anaotaka wasajiliwe ambayo italinganishwa na orodha ya Kamati ya Ufundi.
    “Tutazijadili pamoja ripoti hizo na kuchukua idadi ya wachezaji ambao wanahitajika kwa mujibu wa mahitaji ya kocha. Suala la nani asajiliwe, tutajadili kwa pamoja, Kamati ya Usajili, Kamati ya Ufundi na benchi la Ufundi,”alisema. 
    Poppe alisema orodha ya wachezaji 33 iliyowasilishwa na Kamati ya Ufundi inahusisha wachezaji wa kigeni na wazawa, kati yao wakiwemo ambao wamemaliza mikataba na timu za hapa nyumbani.
    Ukitazama hali halisi ya Simba katika Ligi Kuu msimu huu, unaona kabisa timu inahitaji kuongezewa wachezaji wenye uzoefu na walio tayari kwa mechi za mashindano ili kuweza kushindani mataji ya nyumbani dhidi ya Azam na Yanga, zilizowekeza vizuri katika vikosi vyake.
    Simba SC haihitaji tena wachezaji wa kujaribu – inahitaji wachezaji ambao watasajiliwa na kucheza, ikitokea wameshindwa, iwe bahati mbaya – bahati mbaya kweli.
    Na aina ya wachezaji ambao wanahitajika Simba huwapati bure, lazima utumie fedha kuwapata kwa kuwatoa kwenye klabu zao za sasa.
    Kama katika orodha ya wachezaji 33 waliopendekezwa kwenye Kamati ya Ufundi kuna aina ya wachezaji ambao wanahitajika Simba ni sawa.
    Lakini kama wanaletwa wachezaji wa kujaribu, basi Simba SC itaendelea kusubiri sana kurudi kwenye michuano ya Afrika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BILA KUWEKA FEDHA KWENYE TIMU, SIMBA WATASUBIRI SANA! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top