• HABARI MPYA

    Sunday, May 22, 2016

    RAIS MPYA WA FIFA AWAMWAGIA PONGEZI WABABE WA NCHI YANGA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, ameipongeza timu ya soka Yanga SC ya Dar es Salaam, kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara 2015/16.
    Yanga SC imetwaa ubingwa huo kwa msimu wa pili mfululizo, lakini ikiwa ni mara ya 26 tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara mwaka 1965.
    Katika salamu zake, kupitia barua yake ya Mei 18, 2016 kwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi, Infantino ameelezea ubingwa wa Yanga kwamba umetokana na kazi kubwa inayofanywa na uongozi wa timu hiyo, makocha, wachezaji pamoja na mashabiki.
    Mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC 

    “Yanga ndiyo mabingwa wa Tanzania. Napenda kuchukua nafasi hii kuipongeza Yanga Africans na timu nzima isiyoshindika kwa mafanikio haya makubwa. Taji la Yanga Africans ni matokeo ya mshikamano ulioko ndani ya Yanga Africans,” amesema Infantino katika barua hiyo yenye kichwa cha habari kinachosema: Salamu za Pongezi kwa Yanga.
    Amesema pongezi zake ziende kwa uongozi wa klabu, makocha na benchi nzima la ufundi, wachezaji, madaktari pamoja na mashabiki wote wa Yanga SC.
    “Kwa niaba ya familia ya soka, napenda kuchukua nafasi hii kuishukuru Yanga SC na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa jinsi mnavyopeleka ujumbe chanya wa soka kwa jamii ya michezo,” alisema Infantino katika barua hiyo iliyotua TFF Mei 21, mwaka huu.
    Tayari Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikwisha kuipongeza Yanga ambayo imepewa Kombe na medali kwa wachezaji 24, viongozi saba wa benchi la ufundi na viongozi wanne wa Kamati ya Utendaji na kwa sasa wanasubiri zawadi ya fedha Sh 81,345,723.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RAIS MPYA WA FIFA AWAMWAGIA PONGEZI WABABE WA NCHI YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top