• HABARI MPYA

    Monday, May 30, 2016

    STRAIKA WA JKT RUVU 'AMFUNIKA' NGOMA WA YANGA LIGI KUU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa Abdulrahman Mussa wa JKT Ruvu ameibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa mwezi Mei 2016.
    Mussa katika kinyag'anyiro hicho aliwapiku Donald Ngoma wa Yanga na Ali Nassoro wa Mgambo Shooting. Katika mwezi huo uliokuwa na raundi tatu, Musa alicheza mechi zote tatu za timu yake na kufunga jumla mabao manne; mawili katika kila mechi.
    Kwa kushinda tuzo hiyo ya Mei ambayo ni ya mwisho kwa msimu huu kwa wachezaji bora wa mwezi, Musa atazawadiwa kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) kutoka kwa wadhamini wa Ligi hiyo, kampuni ya Vodacom.
    Donald Ngoma wa Yanga amezidiwa kete na mcgezaji wa JKT Ruvu katika tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu mwezi Mei 

    Washindi wengine wa tuzo hiyo ya mwezi kwa msimu huu wa 2015/2016 ambao mechi zake za mwisho zilichezwa Mei 22 mwaka huu ni Hamisi Kiiza wa Simba (Septemba), Elias Maguli wa Stand United (Oktoba), Thaban Kamusoko wa Yanga (Desemba), Shomari Kapombe wa Azam (Januari), Mohamed Mkopi wa Tanzania Prisons (Februari), Shiza Kichuya wa Mtibwa Sugar (Machi) na Juma Abdul wa Yanga (Aprili).
    Wakati huo huo: Michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) msimu wa 2015/2016 inaendelea vizuri katika vituo vinne vya Kagera, Morogoro, Singida na Njombe ambapo itafikia tamati Juni 6 mwaka huu.
    Timu sita zitapanda daraja kucheza Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu wa 2016/2017. Timu hizo ni zile zitakazoongoza kila kundi, na washindwa bora (best losers) wawili kutoka makundi mawili tofauti.
    Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeweka waangalizi wake katika kila kituo, na litawachukulia hatua watu wote watakaobainika kutumia michuano hiyo kuchafua viongozi.
    Mtwivila City ya Iringa inaongoza kituo cha Njombe ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi tatu. Katika kituo hicho kesho (Mei 31) kutakuwa na mechi kati ya Jangwani FC ya Rukwa na Nyundo FC ya Katavi kwenye Uwanja wa Amani.
    Timu inayoongoza kituo cha Morogoro ni Namungo FC ya Lindi yenye pointi saba kwa mechi tatu. Kesho (Mei 31) ni mechi kati ya Makumbusho FC na Sifapolitan, zote za Dar es Salaam itakayofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
    Kitayose ya Kilimanjaro inaongoza kituo cha Singida ikiwa na pointi tisa baada ya kushinda mechi zote tatu ilizocheza. Kesho (Mei 31) kwenye kituo hicho kutakuwa na mechi kati ya Stand FC ya Tabora na Murusgamba ya Kagera itakayochezwa Uwanja wa Namfua.
    Mpaka sasa vinara wa Kituo cha Kagera ambacho mechi zake zinachezwa Uwanja wa Vijana mjini Muleba ni Mashujaa FC ya Kigoma yenye pointi saba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STRAIKA WA JKT RUVU 'AMFUNIKA' NGOMA WA YANGA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top