• HABARI MPYA

    Sunday, May 22, 2016

    AZAM FC YAIPIKU SIMBA NAFASI YA PILI, TANGA NZIMA YAIPA MKONO WA KWAHERI LIGI KUU

    Na Waandishi Wetu, VITUONI
    AZAM FC imeipiku Simba SC kwa kumaliza nafasi ya pili baada ya mechi za mwisho za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo.
    Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, JKT Ruvu imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba SC, mabao yake yakifungwa na Abdulrahman Mussa dakika ya kwanza na 30, wakati la Wekundu wa Msimbazi limefungwa na Nahodha Mussa Hassan Mgosi dakika ya 70.
    Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam pia, wenyeji Azam FC wamelazimishwa sare ya 1-1 na Mgambo JKT ya Tanga.
    Ramadhani Singano ‘Messi’ alianza kuifungia Azam FC dakika ya 60 kabla ya Fully Maganga kuisawazishaia Mgambo dakika ya 72.
    Kiungo wa Simba, Abdi Banda akipambana katikati ya wachezaji wa JKT Ruvu leo

    Kwa matokeo hayo, Azam FC inamaliza na pointi 64, ikifuatiwa na Simba SC inayomaliza na pointi 62 katika nafasi ya tatu.
    Yanga SC ambayo ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu wiki mbili zilizopita, leo imemaliza kwa sare ya kufungana mabao 2-2 na wenyeji Majimaji Uwanja wa Majimaji mjini Songea hivyo kufikisha pointi 73.
    Mechi nyingine za kufunga pazia la Ligi Kuu, wenyeji Toto Africans wamefungwa 1-0 na Stand United Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Coastal Union wamefungwa 2-0 na Prisons Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Mbeya City imelazimishwa sare ya 0-0 na Ndanda FC, Mtibwa Sugar wameichapa 2-0 African Sport na Kagera Sugar wameshinda 2-0 dhidi ya Mwadui FC.
    Kwa matokeo hayo, timu zote za Tanga, Mgambo JKT, African Sports na Coastal Union zinaipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu, zikizipisha Ruvu Shooting, Mbao FC na African Lyon.  
    Mgambo JKT imemaliza na pointi 28, African Sports 26 na Coastal 22. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAIPIKU SIMBA NAFASI YA PILI, TANGA NZIMA YAIPA MKONO WA KWAHERI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top