TIMU ya Mamelodi Sundowns FC imefanikiwa kwenda Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika licha ya kuchapwa mabao 2-0 na wenyeji, Stade Malien katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali jana Uwanja wa Machi 26 Jijini Bamako nchini Mali.
Mabao ya Stade Malien jana yalifungwa na winga wa kushoto, Mcameroon Taddeus Nkeng Fomakwang dakika ya kwanza na kiungo mzawa, Haman Mandjan dakika ya 40.
Kwa matokeo hayo, Mamelodi Sundowns FC wanakwenda Nusu Fainali kwa ushindi wa jumla wa 3-2 kufuatia kuichapa Stade Malien 3-0 kwenye mchezo wa kwanza wa Robo Fainali Machi 13, mabao yake yakifungwa na beki wa kulia, mzawa, Khuliso Mudau dakika ya 34 na washambuliaji Mcolombia, Brayan León Muñiz dakika ya 54 na mzawa, Iqraam Rayners dakika ya 74 Uwanja wa Loftus Versfeld Jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Nayo RS Berkane ya Morocco ilifanikiwa pia kwenda Nusu Fainali baada ya ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Al-Hilal SC Omdurman Uwanja wa Amahoro Jijini Kigali, Rwanda.
Bao pekee la RS Berkane mabingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita lilifungwa na winga wa kushoto, Mounir Chouiar dakika ya 90’+3 akisawazisha makossa yake baada ya awali dakika ya 61 kukosa penalti.
Kwa matokeo hayo, RS Berkane wanakwenda Nusu Fainali kwa ushindi wa jumla wa 2-1 kufuatia sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Machi 15 Uwanja wa Manispaa ya Berkane Jijini Berkane nchini Morocco, Mounir Chouiar akifunga bao la kusawazisha dakika ya 90+9 baada ya kiungo Abdel Raouf kuanza kuifungia Al Hilal dakika ya 13.
Mechi za kwanza za Nusu Fainali zitachezwa Aprili 10 na marudiano Aprili 17, Mamelodi Sundowns ikimenyana na Esperance ya Tunisia iliyoitoa Al Ahly na RS Berkane ikicheza na ndugu zao wa Morocco, FAR Rabat ambao waliwatoa mabingwa watetezi, Pyramids.



.png)
0 comments:
Post a Comment