• HABARI MPYA

    Sunday, May 29, 2016

    AZAM SASA NDIYO ALAMA YA SOKA YA TANZANIA, TFF ISIPOWASHIKA VIZURI...

    SIKU mbili baada ya kusherehekea kileleni cha michuano ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya miaka kadhaa ya kifo chake, Watanzania wakapokea habari nyingine njema juu ya soka yao.
    Ni ujio wa michuano miwili mipya kabisa katika historia ya soka Tanzania, Ligi Kuu ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 na Ligi Kuu ya Wanawake. 
    TFF Ijumaa iliiingia Mkataba wenye thamani ya Sh. Bilioni 2 na kampuni ya Azam Media Limited walionunua haki za kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania na Ligi Kuu ya Vijana wa umri chini ya miaka 20.

    Zoezi hilo lilifanyika Ofisi za makao Makuu ya Azam Media Ltd eneo la TAZARA, Dar es Salaam upande wa TFF ukiwakilishwa na Rais wake, Jamal Malinzi na Azam Media wakiwakilishwa na Mtendaji wake Mkuu, Muingereza Rhys Torrington.
    Akizungumza katika hafla hiyo fupi, Torrington alisema Mkataba huo ni wa miaka mitano na lengo lao ni kuendelea kusaidia kuinua michezo Tanzania.
    Kwa upande wake, Malinzi alisema kwamba Ligi Kuu ya Wanawake itaanza kwa kushirikisha klabu 10 Agosti mwaka huu na Ligi ya U20 itashirikisha klabu zote za Ligi Kuu ya Wanaume.
    Malinzi alisema Ligi ya Wanawake itaanza na timu 10 baada ya hapo Chama Cha Soka ya Wanawake (TWFA) kitatengeneza muundo wa timu kupanda na kushuka.
    Kuhusu Ligi ya vijana, Malinzi alisema wataunda kanuni kali za Ligi Kuu kuhakikisha klabu zote za ligi hiyo zinashiriki kikamilifu na kwamba klabu itakayoshindwa kuingiza kikosi cha vijana uwanjani itakatwa pointi tatu katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara  
    Azam Media wanaweka mabilioni hayo katika soka ya Tanzania – baada ya kuweka mabilioni mengine mengi katika miradi mbalimbali ya maendeleo ya soka yetu.
    Kurejea kwa Kombe la TFF pia ni kwa sababu ya Azam TV walioweka fedha za udhamini wa michuano hiyo ambayo mara ya mwisho ilifanyika mwaka 2002, JKT Ruvu wakitwaa ubingwa.
    Na wakati wote huo mashindano hayakuwahi kuwa na udhamini wowote ni Azam TV wanakuwa wadhamini wa kwanza kuweka fedha kwenye michuano hiyo.
    Awali ya hapo, Azam TV waliweka mabilioni mengine katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara waliponunua haki za matangazo ya moja kwa moja.
    Hiyo ilikuja baada ya miaka mingi ya Ligi yetu kuonyeshwa kienyeji na baadhi ya Televisheni bila kuilipa TFF wala klabu.
    Sasa Ligi Kuu ya Tanzania imekuwa na hadhi kubwa, pato la klabu limeongezeka kutokana na ongezeko la fedha za Azam.
    Ikumbukwe, kabla ya hapo Azam ambayo inamilikiwa na kampuni ya Bakhresa Group Limited, walianzisha mradi mkubwa wa soka kupitia Azam FC.
    Mradi huo wenye maskani yake eneo la Mbade, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam unahusisha timu ya wakubwa, inayoshiriki Ligi Kuu na timu za vijana zilizopo katika akademi.
    Azam FC ni klabu ya kipekee nchini na ndani ya muda mfupi wa ujio wake, imeleta mapinduzi makubwa katika soka ya Tanzania.
    Akademi yake inazalisha vijana wengi ambao ndani ya muda mfupi wamegeuka kuwa nyota wa taifa, mfano Farid Mussa, Aishi Manula, Simon Msuva na wengine.
    Lakini pia kikosi cha Ligi Kuu cha Azam FC kimeleta changamoto kubwa na kuondoa ukiritimba wa klabu kongwe za Simba na Yanga.
    Sasa Simba na Yanga wanajua kama wanahitaji kushinda mataji nchini, wanatakiwa kuwekeza fedha kwenye timu zao.
    Yanga imeweza kwenda sambamba na Azam FC katika mbio za mataji kwa sasa, kwa sababu inaweka fedha, lakini Simba SC wameshindwa na sasa wamegeuka kuwa timu ya kushiriki Ligi Kuu tu.
    Azam pia wamekuwa wepesi kutoa misaada mbalimbali katika soka yetu, pasipo kujitangaza – dhamira ya wazi ikionekana kusaidia maendeleo ya mchezo nchini.  
    Kwa sasa karibu kila eneo la soka ya Tanzania kuna Azam – kuanzia katika Ligi Kuu, Ligi Kuu ya vijana, Ligi Kuu ya Wanawake na hata timu za taifa.
    Azam si wadhamini wa timu yoyote ya taifa, lakini kwa kuwa sasa wamekuwa tegemeo la kuzalisha wachezaji kuanzia vijana hadi wakubwa, ndiyo maana wapo kote huko.
    Azam sasa ni alama ya soka ya Tanzania – kutokana na kuwa mstari wa mbele kusaidia maendeleo ya soka ya nchi hii.
    Ujio wa Ligi ya Vijana ni mwanzo wa mapinduzi mapya halisi ya soka ya Tanzania, kwani kwa muda mrefu Tanzania imekuwa hodari wa kuvumbua vipaji vya vijana wadogo, lakini tatizo linakuwa katika kuwaendeleza na tumekuwa tukiacha vipaji vingi katikati.
    Sasa ni wazi, baada ya kuibua vipaji vya vijana chini ya umri wa miaka 17 na 15, hatua yao ya pili itakuwa ni kucheza Ligi ya U20 na baada ya hapo wanapanda vikosi vya wakubwa wakiwa wameiva vizuri.
    Naamini hata TFF wanauona sasa umuhimu wa Azam kwao kama wasimamizi wa soka ya nchi hii na umuhimu wa kampuni hiyo kwa mchezo wa mpira wa miguu kwa ujumla nchini.
    Haitoshi kuujua umuhimu tu, bali TFF pia wanapaswa kuwashika vizuri Azam, kwani wakitoweka litakuwa ni pigo kubwa kwa soka yetu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM SASA NDIYO ALAMA YA SOKA YA TANZANIA, TFF ISIPOWASHIKA VIZURI... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top