• HABARI MPYA

    Monday, May 23, 2016

    AYA 15 ZA SAID MDOE: NDI NDI NDI!

    HADI leo bado sijaulewa kabisa wimbo wa “Ndi Ndi Ndi” wa msanii nyota wa kizazi kipya Judith Wambura Mbibo “Lady Jay Dee” au Jide, lakini hiyo haiondoi heshima yangu kubwa niliyoweka kwa mwimbaji huyu. 
    Nimeusikiliza tena na tena lakini licha ya utamu wa mpangilio wa ala na njia tamu za uimbaji alizotumia Jide, lakini bado sikuelewa jina la wimbo limeakisi nini, linahusiana vipi na ujumbe unaopatikana katika wimbo huo.
    Lakini kuna jambo moja kubwa ambalo kwa mara nyingine tena Jide analifanikisha kupitia tungo hii nalo ni kuleta msemo mpya mjini - “Ndi Ndi Ndi”.

    Kama ilivyokuwa kwa wimbo wake wa “Yahaya” au “Siku Hazigandi” ambazo zilizua msemo mpya, ndivyo ilivyo pia kwa neno “Ndi Ndi Ndi” ambalo limekuwa gumzo kila kona hata kwa akina sie tusiojua maana ya “Ndi Ndi Ndi”.`
    Jide si msanii wa kubeza katika midani ya muziki hapa nchini na Afrika Mashari kwa ujumla wake, ni bonge la mbunifu na ndiyo maana ameweza kudumu kwa muda mrefu kwenye ‘game’.
    Tangu aibuke rasmi katika muziki wa kizazi kipya mwaka 1999 na hatimaye kuachia albam yake ya kwanza “Machozi”, mwaka 2000, mwanadada huyu hajawahi kukauka au kuishiwa kisanii, amekuwa kwenye kilele cha mafanikio mwaka hadi mwaka.
    Moja ya vitu vilivyozidi kudhihirisha ubunifu wa Jide ni onyesho lake la “Naamka Tena” lililofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam Ijumaa iliyopita.
    Ilikuwa ni bonge la show iliyothibitisha kuwa Jide si mwimbaji wa kuchovya, bali ni msanii aliyekamilika mwenye uwezo wa kupiga muziki wa ‘live’ na sio ule wa ‘playback’ wa kuweka CD kisha msanii anakandamizia juu yake.
    Ilikuwa ni show iliyodhihirisha (japo kwa mlango wa uani) kuwa muziki wa dansi bado uko hai na kinachotakiwa ni ubunifu tu.
    Jide aliuenzi vema muziki wa dansi katika onyesho hilo ambapo nyimbo zake tatu alizozirudia upya kutoka kwa wakongwe wa dansi, ndizo zilizoteka show kwa kiasi kikubwa.
    Nyimbo kama “Shida” wa Mbaraka Mwishehe na “Siwema” na “Ndoa ya Mateso” za Marijan Rajab, ziliamsha shangwe kubwa Mlimani City, jambo lililotoa picha kuwa kama wasanii wote wa kizazi kipya watafuata nyayo za Jide, basi muziki wa dansi hautapotea milele na milele.
    Jide alifanya ubunifu wa kuweka ‘sebene’ fulani kwenye kwenye nyimbo zake zote na kuufanya muziki wake unyanyue mashabiki wengi kwenye viti vyao – alitumia mirindimo na vionjo vingi vya muziki wa dansi kuboresha onyesho lake.
    Kuna darasa kubwa kwa wanamuziki wa dansi na wa bongo fleva kupitia onyesho la Jide – kwamba hakuna haja ya kuwekeana matabaka na badala yake suala la kubadilishana ujuzi lichukue nafasi.
    Wanamuziki wa dansi wajifunze namna ya kuboresha soko lao kupitia wasanii wa bongo fleva na wakati huo huo wasanii hao wa bongo fleva nao wajifunze kupiga muziki wa ukweli kutoka kwa wanamuziki wa dansi ili wawe warithi wa baadae.
    Bila juhudi za makusudi, nchi yetu itakuwa hatarini kuingia kwenye uhaba wa wanamuziki wenye uwezo wa kutumia ala za muziki na badala yake tutabakiwa na wacheza CD peke yake.
    Kwa miaka mingi, Lady Jay Dee amekuwa akihakikisha anafanya maonyesho yake kwa kutumia bendi (live) na Ijumaa iliyopita akadhihirisha kuwa muziki wa bendi una nguvu. NDI NDI NDI!
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AYA 15 ZA SAID MDOE: NDI NDI NDI! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top