• HABARI MPYA

    Wednesday, May 25, 2016

    TUZO ZA TASWA KUTOLEWA AGOSTI 26 DAR

    Na Renatha Msungu, DAR ES SALAAM
    SHEREHE za tuzo za Wanamichezo Bora zinazotolewa kila mwaka na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA zitafanyika Agosti 26, mwaka huu mjini Dar es Salaam. Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA kilichofanyika jana mjini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, Juma Abbas Pinto.Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari leo kwamba chama kimeuanda kamati maalum kwa ajili ya kusimamia upatikanaji wa wanamichezo hao bora.
    Rais mstaafu, Dk Jakaya Mrisho Kikwete(wa pili kushoto) akipokea tuzo maalum ya mchango wake mkubwa katika sekta ya michezo katika kipindi cha miaka yake 10 ya utawala wake, kutoka kwa Mwenytki wa TASWA, Juma Pinto (wa pili kulia). Wengine pichani ni aliyekuwa Waziri wa Michezo, Dk Fenella Mukangara (kushoto) na Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi (kulia)

    Mhando, Mhariri wa magazeti ya Serikali, Daily News, Habari Leo na Spoti Leo,  amesema kwamba kamati hiyo inajumuisha waandishi waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya habari na wataalamu kutoka vyama mbalimbali vya michezo, Sekretarieti ya TASWA ikiendelea kuwasiliana na wateule wa kamati hiyo kabla ya kuwatangaza.
    TASWA hutoa tuzo kwa wanamichezo bora wa kila mchezo na pia kunakuwa na mwanamichezo bora wa jumla kwa mwaka husika.
    Baadhi ya waliopata kutwaa tuzo ya Mwanamichezo Bora Tanzania wa jumla kwa miaka kumi iliyopia na miaka yao katika mabano ni Samson Ramadhani (2006), Martin Sulle (2007) na Mary Naali (2008) wote wanariadha.
    Mwaka 2009 tuzo ilienda kwa mcheza netiboli Mwanaidi Hassan, ambaye pia alitwaa tuzo hiyo mwaka 2010, wakati mwaka 2011, ambapo tuzo yake ilitolewa mwaka 2012 mshindi alikuwa mwanasoka Shomari Kapombe. Mwaka 2013/2014 ilienda kwa mwanasoka Sheridah Boniface.
    Mwaka 2015 tuzo ilifanyika katika aina nyingine,  ambapo walizawadiwa wanamichezo 10 tu waliofanya vizuri zaidi katika miaka 10 ya urais wa Jakaya Kikwete na pia TASWA ilitoa Tuzo ya Heshima kwa Kikwete.
    Kuhusu tamasha la Siku ya Vyombo vya Habari, maarufu kama Media Day Bonanza, Mhando amesema; "Kama inavyojulikana chama chetu kimekuwa kikiandaa bonanza maalum likihusisha waandishi na wafanyakazi wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini, lakini kwa miaka miwili bonanza hilo limekwama kufanyika kutokana na sababu mbalimbali,". 
    "Kikao kimekubaliana nguvu zaidi ielekezwe ili jambo hilo lifanyike na kuwapa raha wadau. Taarifa zaidi kuhusu Media Day itatolewa Jumamosi wiki hii," amesema.
    (Renatha Msungu ni mwandishi wa gazeti la Nipashe)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUZO ZA TASWA KUTOLEWA AGOSTI 26 DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top