• HABARI MPYA

  Thursday, March 17, 2016

  KADI ZAMPONZA KESSY KUIKOSA SIMBA NA COASTAL JUMAMOSI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  VINARA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC wameondoka Dar es Salaam jioni hii kwenda Tanga kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi dhidi ya wenyeji Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Kocha Mganda, Jackson Mayanja amemuacha Dar es Salaam beki tegemeo Hassan Ramadhani Kessy kwa sababu anatumikia adhabu ya kadi, wakati beki Mohammed Faki na mshambuliaji Hajji Ugando ni majeruhi.
  Ikumbukwe, beki mwingine wa kati Hassan Isihaka amefungiwa jana mwezi mmoja kwa kosa la utovu wa nidhamu – hivyo naye pia hayumo safarini.
  Simba SC itacheza mechi yake ya 24 Jumamosi na kufikisha idadi ya mechi tatu za kuwazidi washindani wake katika mbio za ubingwa, Azam na Yanga.
  Hassan Kessy hatakuwepo Jumamosi Yanga ikimenyana na APR

  Na Wekundu hao wa Msimbazi ndiyo wanaongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 54, nne zaidi ya Yanga na Azam FC ambao wikiendi hii watakuwa na mechi za michuano ya Afrika.
  Yanga watakuwa wenyeji wa APR ya Rwanda katika mchezo wa marudiano wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kushinda 2-1 mjini Kigali Jumamosi iliyopita.
  Azam FC watakuwa wenyeji wa Bidvest Wits ya Afrika Kusini Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kushinda 3-0 mjini Johannesburg Jumamosi iliyopita.
  Lakini kwa ujumla Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itaendelea wikiendi hii na mbali na mchezo wa Coastal na Simba keshokutwa – kesho Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
  Mechi nyingine za Jumamosi ni kati ya Majimaji na Mbeya City Uwanja wa Majimaji, Songea, Stand United na Ndanda FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga wakati Jumapili African Sports watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mkwakwani na Jumatatu Mgambo watamenyana na Toto Africans.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KADI ZAMPONZA KESSY KUIKOSA SIMBA NA COASTAL JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top