• HABARI MPYA

    Sunday, March 27, 2016

    KAZI ILIFANYIKA D'JAMENA, LAKINI SHUGHULI BADO PEVU STARS

    Na Prince Akbar, ALIYEKUWA D'JAMENA
    MJUMBE wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Pelegrinius Rutayuga alitangulia mjini D’jameda wiki moja kabla ya mchezo kwenda kuandaa mazingira ya timu ya taifa, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa Kundi G, kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika 2017.
    Rutayuga alitekeleza wajibu wake vizuri kwa kuipatia kambi nzuri timu katika hoteli bora zaidi mjini humo, Ledger Plazza na kuandaa mapokezi ya timu itakapowasili kwa maana ya usafiri na hadi mipango ya maisha ya timu mjini humo kwa ujumla.
    Taifa Stars ililazimika kuondoka kwa makundi mawili Dar es Salaam kutokana na baadhi ya wachezaji kuwa bado wana majukumu ya klabu zao na kundi la kwanza liliwasili Jumatatu mjini D’jamena na kupokewa vizuri na Ruta.
    Mshambuliaji wa Tanzania, Thomas Ulimwengu aliipa misukosuko ya kutosha safu ya ulinzi ya Chad D'jamena

    Kundi hilo la kwanza lilihusisha wachezaji wafuatao; Ally Mustafa 'Barthez', Juma Abdul, Haji Mwinyi, kelvin Yondani, Deus Kaseke, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Ibrahim Hajib, Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim na Nahodha Mbwana Samatta.
    Kundi la pili lilimhusisha mshambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu na wachezaji wa Azam FC ambao ni kipa Aishi Manula, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni na David Mwantika, viungo Himid Mao na Farid Mussa na mshambuliaji John Bocco.
    Wakati Ulimwengu alichelewa kutokana na kuwa anaitumikia klabu yake, Mazembe Jumapili katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St George ya Ethioppia, wachezaji wa Azam nao walikuwa wana mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini siku hiyo pia Dar es Salaam. Timu zote, Mazembe na Azam FC zimefuzu hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo ya Afrika.
    Siku moja kabla ya mechi, yaani Jumanne ndipo wachezaji wote wa Stars walifanya mazoezi kwa pamoja ambayo yalikuwa mepesi tu kwa sababu yalikuwa ya mwisho kabla ya mechi hiyo. 
    Hali ya joto kali la Chad zaidi ya nyuzi 42 liliwalazimu wachezaji hao kunywa maji mara kwa mara wakati wa mazoezi yao kwenye Uwanja wa nyasi bandia zilizochakaa zenye kuunguza ile mbaya.
    Hoteli ya Ledger Plaza mjini D'jamena ambayo Taifa Stars walifikia
    Rutayiga (kulia) alifanya kazi nzuri baada ya kutangulia D'jamena

    Na siku iliyofuata mchezo ulipigwa katika jua kali la Alasiri, lakini wachezaji wa Stars walijituma na kufanikiwa kuibuka na ushindi, bao pekee la Nahodha, Samatta dakika ya 30 aliyemalizia krosi ya winga chipukizi, Farid Mussa Malik.
    Baada ya mchezo huo, wachezaji walirejea hotelini Ledger Plaza kwa mapumziko kabla ya mchana wa Alhamisi kuanza safari ndefu kidogo ya kurejea nyumbani kupitia Addis Ababa.
    Ndege ya shirika la Ethiopia iliruka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hassan D’jamous Saa 8:15 mchana kwa saa za Chad, saa mbili zaidi kwa Tanzania na ilitua Addis Ababa Saa 2:00 usiku. Wachezaji wa Stars walikaa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole mjini Addis Ababa hadi Saa 5:00 usiku walipounganisha ndege nyingine ya Ethiopian Airlines kurejea Dar es Salaam, walipofika Saa 8:02 usiku.
    Iliwachukua takriban saa moja hadi kutoka Uwanja Ndege wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kuelekea hotelini, Urban Rose, katikati ya Jiji, ambako waliungana na wachezaji waliobaki, kipa Shaaban Kado, viungo Ismail Khamis ‘Suma’, Said Ndemla na washambuliaji Elias Maguri, Jeremiah Juma na Abdillah Yussuf ‘Adi’. 
    Ijumaa jioni wachezaji wote wa Stars walifanya mazoezi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kasoro beki Kevin Yondan na kiungo Mwinyi Kazimoto ambao waliumia katika mchezo wa kwanza. Wakati Kazimoto alicheza kwa dakika 45 na kushindwa kuendelea, Yondan alijitutumua na kumaliza dakika 90, lakini baada ya mechi alikimbizwa hospitali mjini D’jamena kwa matibabu.
    Mbwana Samatta (kushoto) akipongezana na Farid Mussa aliyempa pasi ya bao pekee D'jamena

    Mchezo wa marudiano utachezwa Jumatatu na Stars inahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kucheza AFCON za pili kihistoria baada ya zile za mwaka 1980 nchini Nigeria.
    Stars inashika nafasi ya tatu katika Kundi G, ikiwa na pointi nne baada ya kushinda mechi moja dhidi ya Chad, kufungwa na Misri 3-0 na kutoa sare ya 0-0 na Nigeria.
    Misri inaongoza Kundi hilo kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na Nigeria yenye pointi nne sawa na Tanzania, lakini ina wastani mzuri wa mabao, wakati Chad inashika mkia haina pointi. Safari bado ndefu kwa Stars, Mungu ibariki Tanznaia, ibariki Taifa Stars. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAZI ILIFANYIKA D'JAMENA, LAKINI SHUGHULI BADO PEVU STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top