• HABARI MPYA

    Monday, March 21, 2016

    YANGA WAIKALIA KIKAO AL AHLY

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm kesho anatarajiwa kuwasilisha programu yake ya maandalizi ya mchezo dhidi ya Al Ahly ya Misri katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Yanga itamenyana na wababe wao wa kihistoria katika michuano ya Afrika, Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Aprili 9, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana Aprili 19, Cairo, Misri.
    Na baada ya Ahly kuinyanyasa kwa miaka mingi Yanga kwenye michuano yote ya CAF, safari hii wana Jangwani wamepania kuvunja mwiko kwa kuhakikisha wanawang’oa Waarabu hao.
    Kocha Hans van der Pluijm kesho anatarajiwa kukabidhi programu ya maandalizi dhidi ya Al Ahly

    Na kesho, Kamati ya Mashindano chini ya Mwenyekiri wake, Isaac Chanji itakutana na benchi la Ufundi chini ya kocha Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi kujadili programu ya maandalizi.
    Lakini tayari programu hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ratiba za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup – maana yake Yanga haiwezi kwenda kuweka kambi nje ya mji.
    Dhamira ya Yanga ilikuwa ni kwenda kuweka kambi Pemba, lakini Machi 31 wana mechi ya Kombe la TFF na Aprili 2 wana mechi ya Ligi Kuu, hivyo watalazimika kubaki Dar es Salaam.
    Na Dar es Salaam japokuwa wanaweza kupata hoteli nzuri ya kuweka kambi, lakini tatizo ni Uwanja mzuri wa mazoezi, kutokana na kukataliwa kufanya mazoezi Uwanja wa Taifa.
    Ahly imefuzu hatua hii baada ya kuitoa Recreativo do Libolo ya Angola kwa ushindi wa jumla wa 2-1, iliyoupata Cairo baada ya sare 0-0 Angola, wakati Yanga imeitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2 ikishinda 2-1 Kigali na kulazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
    Mara ya mwisho timu hizo zilikutana mwaka 2014 katika Raundi ya Kwanza na Yanga ikatolewa kwa penalti 4-3, baada ya sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAIKALIA KIKAO AL AHLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top