• HABARI MPYA

    Monday, March 28, 2016

    CHOYO, FITNA, WOGA NA UBAGUZI DONDA NDUGU LA MUZIKI WA DANSI

    Nimehudhuria onyesho la Twanga Pepeta na Mashauzi Classic pale Mango Garden usiku wa kuamkia leo, nikabaki na maswali mengi juu ya mwelekeo wa muziki wa dansi.
    Wakati muziki wa kizazi kipya ulipoanza kubisha hodi enzi za radio moja (Radio Tanzania Dar es Salaam – RTD) mwanzoni mwa miaka ya 90, ulionekana wa kihuni ukatiwa kapuni, muziki wa dansi ukaendelea kupeta raha mustarehe.
    Hata pale Radio One Stereo ilipoanzishwa mwaka 1994 huku Taji Liundi “Master T” akiubebea bango muziki wa kizazi kipya na hatimaye kuzaliwa kwa kipindi cha DJ Show kilichogeuka kuwa mbeleko kubwa ya muziki huo, hakuna mtu wa muziki wa dansi aliyeshtuka zaidi ya kauli ile ile ya “Muziki wa kihuni”.

    Mtangazaji mwingine wa Radio One aliyerithi nafasi ya Taji Liundi, Mike Mhagama naye akawa chachu kuupaisha muziki wa kizazi kipya na kupitia yeye jina la “Bongo Fleva” likazaliwa, kilichofuata baada ya hapo ni kila kituo kipya binafsi kilichozaliwa kikawa na programu ya Bongo Fleva. Muziki wa dansi ukaendelea kujiamini.
    Miaka 20 baadae muziki uliokuwa na nguvu zaidi Tanzania – muziki wa dansi unalalamika kuwa Bongo Fleva inabebwa. Ni kweli kabisa muziki wa dansi unafukiwa na media, ni kweli bongo fleva inakumbatiwa na media hakuna ubishi katika hilo, lakini ni pia ni ukweli usiopingika kuwa muziki wa dansi ulilemaa, ukabweteka, ukalala usingizi.
    Bongo Fleva ilikuwa ikijitanua hatua kwa hatua, muziki wa dansi ukawa unasinyaa hatua kwa hatua lakini hakuna aliyeona - kinachofanywa sasa hivi na muziki dansi ni sawa kabisa na serekali inayoacha kibanda cha kwanza kinajengwa bondeni, cha pili, cha tatu hakuna katazo wala bomoa bomoa hadi kinazaliwa kitongoji kikubwa chenye vibanda vingi na familia kibao ndipo inaamka na kuanza bomoa bomoa.
    Tuachane na Bongo Fleva, tuangalie muziki wa taarab ambao zamani ilikuwa ni kama ‘haramu’ kuupiga kwenye vituo binafsi vya radio lakini leo hii unachanua kila kona si kwenye TV wala radioni, kwanini? Ni kwasababu taarab wanakwenda na mabadiliko kutokana na mahitaji ya soko.
    Taarab ilifanyiwa mabadiliko makubwa mwanzoni mwa miaka ya 90 na kuzaliwa kitu kinaaitwa “Modern Taarab” na kutoka hapo ikawa inaendelea kuongezwa vitu kila kukicha na kuutoa muziki huo kutoka muziki wa kusikiliza hadi kuwa muziki wa kucheza.
    Leo unajiuliza nini kimetokea hadi muziki wa dansi kuwa wa kusikiliza na taarab kuwa muziki wa kucheza, bendi nyingi (si zote) zinakosa tungo na mirindimo itakayomlazimisha mtu aache kiti chake na kwenda kucheza - ukiuliza wadau utakutana na majibu mepesi mepesi na wala hakuna anayekerwa na hali hiyo.
    Kwa muda mrefu Jahazi Modern Taarab chini yake Mzee Yussuf imekuwa ikilishika soko la muziki wa dansi na taarab, imekuwa na wateja wengi kwenye maonyesho yao kuliko bendi yoyote ya dansi na taarab (ukiondoa ujio wa Malaika Band). Kwanini? Ni kwasababu imefanikiwa pia kuiba mashabiki muziki wa dansi wanaotaka kucheza na si kusikiliza au kutazama show na hicho ndicho kinachofanywa na bendi zote kubwa za taarab.
    Show ya Mashauzi Classic na Twanga Pepeta ndani ya Mango Garden ni kielelezo kizuri cha namna taarab ilivyo na athari kubwa, mashabiki wanakwenda kucheza na kuijaza kabisa ‘dancing floor’ bila kulazimishwa, bila kuhimizwa, bila kuhamasishwa.
    Wakati Mashauzi Classic walipomaliza ngwe yao ya pili, wakapanda Twanga Pepeta kumalizia show ratiba ya onyesho hilo na kilichoonekana jukwaani ni kama vile walipata somo fulani kwenye taarab ambapo rapa Ferguson akaanza kuhimiza watu waende mbele kucheza, ikawa kama kapata aina fulani ya rap vile … “njooni mbele, njooni wote tucheze, njooni mbele, njooni wote tucheze” akarudia tena na ndipo mashabiki walipoanza kuinuka na kwenda kucheza lakini bado hawakufikia kijiji kilichokusanywa na Isha Mashauzi.
    Ipo haja ya watu muziki wa dansi kujiangalia mara mbili mbili kuanzia tungo zao hadi mpangilio wa muziki, kwanini watu wacheze nyimbo za Yamoto, nyimbo za Kiba, Diamond, Njenje, nyimbo za taarab? Kwanini nyimbo zao hazitesi kwenye maharusi na sherehe zingine? Kwanini nyimbo za Bella anayetengwa kiaina na watu dansi zichezeke, zitawale kila kona? Kwanini nyimbo za zamani za Msondo na Sikinde zinawainua watu vitini?
    Ifike wakati sasa watu dansi wazike choyo, fitna, woga na ubaguzi na badala yake wabakie na kitu kimoja tu – wivu wa maendeleo. Wajifunze na wanyofoe vitu kutoka kwenye aina nyingine ya muziki unaokubalika na kuuchanganya kwenye muziki wao.
    Tunaambiwa siku zote mtu unayehisi kakuzidi nguvu ungana nae, ukitaka kupambana basi yanaweza yakazaliwa mengi hadi imani za kishirikina, hata gitaa lako likikoroma utasema umelogwa. Ni hayo tu, najua nimetibua mzinga wa nyuki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHOYO, FITNA, WOGA NA UBAGUZI DONDA NDUGU LA MUZIKI WA DANSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top