• HABARI MPYA

    Wednesday, March 30, 2016

    MISS TANZANIA WA ZAMANI AIPA SOMO SERIKALI

    Na Somoe Ng'itu, DAR ES SALAAM
    MISS Tanzania (2001) na mwanamitindo wa kimataifa, Millen Happiness Magese, ameiomba serikali kuwekeza katika vifaa vya tiba ya ugonjwa wa Endometriosis ili kuepusha wasichana wa Kitanzania wasipate hali ya ugumba ambao unamkabili na kumuumisha katika maisha yake ya kila siku.
    Akizungumza katika semina maalum iliyoshirikisha zaidi ya wanafunzi 400 wa kike wa Shule za Sekondari mbalimbali jijini Dar es Salaam, Millen alisema kwamba endapo serikali itaongeza nguvu kupata vifaa hivyo, itasaidia kupunguza tatizo hilo linalowakabili mamilioni ya wanawake duniani.
    Mwanamitindo wa kimataifa, Millen Happiness Magese akizungumza na wanafunzi wa sekondari ya Turiani, Magomeni, Dar es Salaam leo kuhusu ugonjwa wa Endometriosis 
    Naibu Waziri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Khamisi Kigwangala akizungumza kwenye hafla hiyo
    Millene na Waziri Kigwangala katika picha ya pamoja na wadau wengine baada ya shughuli hiyo
    Millene akipiga picha na wanafunzi wa sekondari ya Turiani leo Magomeni

    Millen alisema kwamba serikali pia ikiandaa programu za mafunzo, itasaidia kutoa elimu kuhusiana na ugonjwa huo ambao huchukua kati ya miaka 7 na 10 kwa mgonjwa kugundulika na kuacha tabia ya wazazi kuona maumivu ya tumbo kwa mabinti zao wakati wa siku za hedhi ni ya kawaida.
    "Mimi dada yenu hapa ni mhanga wa ugonjwa huu, inaniuma sana, ndoto zangu za kuwa mama zimekwama, naomba serikali iweke mkazo katika kupatikana kwa vifaa vya matibabu ili wasichana na wanawake ambao wengi ni nguvu kazi ya taifa wasipate madhara ambayo mimi nimeyapata na ninaendelea kuumia," alisema mrembo huyo.
    Naibu Waziri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Khamisi Kigwangala aliahidi serikali imejipanga kuhakikisha inaboresha  sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma zilizo bora na kwa wakati muafaka.
    Kiongozi huyo alimpa pole mrembo huyo kwa kuweka wazi tatizo lake na kumtaka asikate tamaa licha ya kufanya upasuaji mara 13 wa kutibu ugonjwa huo na bado hajafanikiwa kupata ujauzito.
    Millen aliongozana na baadhi ya warembo wenzake ambao waliwahi kutwaa taji la Miss Temeke akiwamo, Jokate Mwegelo pamoja na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Judith Wambura 'Lady Jay Dee'.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MISS TANZANIA WA ZAMANI AIPA SOMO SERIKALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top