• HABARI MPYA

  Thursday, March 17, 2016

  JUMA ABDUL NJE YANGA NA APR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA itamkosa beki wake aliye katika kiwango kizuri kwa sasa, Juma Abdul Jaffar katika mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya APR ya Rwanda Jumamosi.
  Mfungaji huyo wa bao la kwanza katika ushindi wa 2-1 dhidi ya APR Jumamosi iliyopita mjini Kigali, ataukosa mchezo wa marudiano kwa sababu atakuwa anatumikia adhabu ya kadi za njano.
  Na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm hana shaka kwa sababu Mkongomani Mbuyu Twite ataziba pengo la Juma Abdul dhidi ya timu yake ya zamani.
  Juma Abdul kushoto atakosekana Yanga na APR Jumamosi

  Yanga inahamishia mazoezi yake Uwanja wa Taifa kwa maandalizi ya mwishoni na Pluijm amesema katika mchezo huo watashambulia kusaka mabao zaidi.
  APR tayari imewasili Dar es Salaam tangu mchana wa leo na kesho jioni itafanya mazoezi Uwanja wa Taifa. 
  APR imekuja na wachezaji ambao ni makipa; Ndoli Jean Claude na Kwizera Olivier. Mabeki Rusheshangoga Michael, Emiry Bayisenge, Rwatubyaye Abdul, Rutanga Eric, Nshutinamara Ismael, Usengimana Faustin na Rwigema Yves. Viungo; Yannick Mukunzi, Iranzi Jean Claude, Patrick Sibomana, Djihadi Bizimana, Benedata Jamvier, Fiston Nkinzingabo na Ntamuhanga Tumaini, wakati washambuliaji ni; Bigirimana Issa, Mubumbyi Barnabe na Bertrand Iradukunda.
  Tayari viingilio vya mchezo huo vimetajwa na wenyeji, Yanga ambavyo ni Sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya Chungwa, Bluu na Kijani, Sh. 25,000 kwa VIP A na 20,000 kwa VIP B na C – tiketi zitaanza kuuzwa mapema siku ya mchezo, Jumamosi katika maeneo ya siku zote, ikiwemo Uwanja wa karume na Uwanja wa Taifa. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: JUMA ABDUL NJE YANGA NA APR Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top