• HABARI MPYA

    Saturday, March 26, 2016

    KAWEMBA AENDA 'KULA NONDO' CAPE TOWN

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    OFISA Mtendaji Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Saad Kawemba, amefunga safari hadi jijini Cape Town Afrika Kusini kushuhudia michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 19 inayoitwa ‘Metropolitan U-19 Premier Cup.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo, Kawemba amesema akiwa huko anatarajia kuzungumza na waandaaji wa michuano hiyo ili kuiwezesha Azam Academy iweze kupata ushiriki wa michezo hiyo mwakani.
    “Tunataka kuipeleka kwenye ramani nyingine kabisa academy yetu ya Azam FC, hivyo niko huku kushuhudia michuano hiyo ya vijana na kuangalia uwezekano wa kuileta academy yetu mwakani,” alisema.
    Saad Kawemba wa pili kulia akiwa mjini Cape Town, Afrika Kusini kushuhudia michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 19 inayoitwa ‘Metropolitan U-19 Premier Cup

    Mbali na kukutana na waandaaji, pia Kawemba atakutana na viongozi wa klabu za Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) pamoja na wale klabu ya Swansea City ya England, ambao wameipeleka academy yao ikashiriki michuano hiyo.
    Kawemba alisema kuwa lengo la michuano hiyo ni kutoa nafasi kwa wasaka vipaji (maskauti) kuwaona vijana wengi kwa wakati mmoja wanapocheza uwanjani ili kuvuna vipaji na kusajiliwa na timu kubwa barani Ulaya na ndani ya Afrika Kusini.
    Azam FC ndio timu pekee hapa nchini iliyofanya uwekezaji mkubwa kwenye eneo la academy, ambayo huwa na programu maalum za kila siku chini ya makocha wenye ujuzi wa kulea vipaji hivi sasa akiwepo Mwingereza Tom Legg akisaidiwa na Mzawa Idd Cheche.
    Mbali na baadhi ya wahitimu wa academy hiyo kusambaa kwenye timu mbalimbali nchini, Azam FC ndani ya kikosi chake cha wakubwa imewavuna nyota kadhaa ambao ni kipa bora kabisa nchini kwa sasa Aishi Manula ‘Tanzania One’, mabeki Abdallah Kheri, Gadiel Michael, viungo Mudathir Yahya, Farid Mussa.
    Wengine walioko timu kubwa waliotolewa kwa mkopo ni beki Ismail Gambo ‘Kusi’ (Mwadui), viungo Omary Wayne (African Sports), Bryson Raphael (Ndanda), Joseph Kimwaga (Simba) na mshambuliaji Kelvin Friday (Mtibwa Sugar).

    Metropolitan U-19 Premier Cup ni nini?
    Michuano hiyo imetimiza miaka 25 tokea ilipoanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1991, ambapo kwa mwaka huu imeandaliwa jijini Cape Town kwenye viwanja vya Erica Park ndani ya Academy ya timu ya Bayhill United, ikiwa inashirikisha jumla ya timu bora za vijana 32 ndani ya mipaka ya Afrika Kusini na nje ya mipaka yao.
    Michuano hiyo ambayo hufanyika ndani ya wiki ya pasaka kwa siku sita, imeshirikisha academy za baadhi ya timu kubwa Ulaya ambazo ni Swansea City, Southampton zote za Uingereza na Juventus ya Italia pamoja na ile ya Zesco United.
    Kihistoria michuano hiyo iliyoanza Jumatano iliyopita hadi Jumatatu ijayo, ndio iliyowatoa wachezaji waliotisha nchini humo hadi kuitwa timu ya Taifa ‘Bafana Bafana’ na kupata soko Ulaya wakiwemo straika hatari Benny McCarthy, Mathew Booth na Mark Williams.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAWEMBA AENDA 'KULA NONDO' CAPE TOWN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top