• HABARI MPYA

    Wednesday, March 30, 2016

    KWELI NI NGUMU, LAKINI NAFASI BADO IPO

    TIMU ya taifa ya Chad imejitoa kwenye mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2017, siku moja kabla ya mchezo wake wa marudiano na wenyeji, Tanzania, Taifa Stars uliokuwa uchezwe juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kwa mujibu wa barua yao kwenda Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Chad wamejitoa kwa sababu za kiuchumi kwamba hawana fedha za kuwawezesha kuendelea na mechi za Kundi G, baada ya kukamilisha mechi tatu za mzunguko wa kwanza, ikifungwa zote, 2-0 na Nigeria ugenini, 5-1 na Misri nyumbani na 1-0 na Tanzania nyumbani Jumatano iliyopita.
    Kujitoa kwa Chad ni hasara kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilioingia gharama za maandalizi ya mchezo wa marudiano, ikiwemo kuandaa tiketi za mchezo.

    Kama Chad wangekuwa na majibu ya mapema japo baada ya mchezo wa kwanza tu D’jamena, TFF isingeingia gharama za ziada na ingevunja kambi, au ingeandaa mchezo wa kirafiki.
    Lakini pia kujitoa kwa Chad ni kama kumewakatisha tamaa wachezaji wa Taifa Stars na hata viongozi wa TFF na wananchi pia, wakiamini hiyo ndiyo ilikuwa timu pekee dhaifu ambayo wangeweza kunufaika kwa kuvuna pointi kwa urahisi.
    Baada ya Chad kujitoa CAF imeitoza faini ya dola za Kimarekani 20,000 na kuifungia kucheza mechi za kufuzu fainali zikazofuata za AFCON – lakini pia matokeo yake yote Kundi G yamefutwa na sasa inahesabika kundi hilo lina timu tatu tu, Misri, Nigeria na Tanzania.   
    Timu zote hizo zimepokonywa pointi zilizovuna kwa Chad, tatu kila timu na Misri iliyovuna ushindi wa mabao 5-1 tofauti na Nigeria waliyovuna 2-0 na Tanzania 1-0, ndiyo muathirika mkuu wa jasho lake la uwanjani.
    Baada ya ushindi wa jana wa Misri 1-0 dhidi ya Nigeria mjini Cairo, Mafarao ndiyo wanaongoza Kundi G kwa pointi zao saba, wakifuatiwa na Nigeria pointi mbili, wakati Taifa Stars ina pointi moja.
    Misri inaweza kumaliza na pointi 10, iwapo itaifunga na Tanzania Juni 4. Tanzania inaweza kumaliza na pointi saba iwapo itashinda mechi zake zote mbili zijazo dhidi ya Misri Juni 4 na Nigeria Septemba 2. 
    Lakini baada ya bao pekee la Ramadan Sobhi kuipa ushindi wa 1-0, Uwanja wa Borg El Arab mjini Cairo, Nigeria ni kama imeaga mashindano.
    Bao hilo la kiungo huyo mshambuliaji wa Al Ahly linaifanya Nigeria ibaki na pointi zake mbili, hivyo kupoteza nafasi ya kwenda AFCON ya Gabon mwakani hata wakiifunga Tanzania katika mchezo wake wa mwisho Septemba 2. 
    Misri itakuja Dar es Salaam kutafuta sare kwa Tanzania ili kujihakikishia kufuzu.
    Tanzania inashika mkia katika Kundi G, lakini ina michezo miwili mkononi dhidi ya zote, Misri nyumbani na Nigeria ugenini.   
    Leo nataka kuwaonyesha Watanzania wenzangu kwamba Stars bado ina nafasi ya kwenda AFCON pamoja na vibonde Chad kujitoa, iwapo tu itashinda mechi mbili zilizobaki.
    Maana yake, TFF, benchi la Ufundi la Taifa Stars na wachezaji kwa pamoja hawapaswi kukata tamaa, badala yake wajipange zaidi kwa ajili ya mechi ambazo wanaamini ni ngumu, kwani bado nafasi ya kwenda Gabon wanayo. 
    Wanachotakiwa kwa sasa ni kujipanga ili wamfunge Misri kwanza katikati ya mwaka, jambo ambalo wengi wanaamini ni gumu.
    Misri watakuja kutafuta sare tu Dar es Salaam ili wafunga mlango wa Kundi G kufuzu AFCON wao wakiwa tayari wamekwishatoka.
    Lakini pamoja na ugumu huo, inaonekana kabisa sasa Tanzania angalau ina wachezaji wa kuunda Taifa Stars ambayo kama itaandaliwa vizuri Misri atafungwa.
    Kwanza ni kumfunga Misri hapa, na si lazima mvua ya mabao, hata 1-0 na baada ya hapo watajua cha kwenda kufanya Nigeria.
    Wazi Nigeria baada ya kupoteza nafasi ya kwenda AFCON tayari moto utawaka, kocha Samson Siasia anaweza kufukuzwa na wachezaji morali itashuka.
    Hakuna uhakika kama hata Shirikisho la Soka Nigeria (NFA) litaipa uzito mechi yake ya mwisho na Taifa Stars, kwa sababu haina faida kwao.
    Sana Nigeria sasa wataelekeza nguvu zao katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2018, ambayo tayari wamefuzu hatua ya makundi ambayo yatapangwa Juni 24 mjini Cairo, Misri.
    Kweli ni ngumu kuwapiku Misri kwenda Gabon, lakini nafasi bado ipo, ni TFF, benchi la ufundi na wachezaji tu kujipanga pasipo kutokata tamaa, ili wawe tayari kupambana, kwani kwenye soka lolote hutokea. Mungu ibariki Tanzania, ibariki Taifa Stars. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWELI NI NGUMU, LAKINI NAFASI BADO IPO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top