• HABARI MPYA

  Saturday, March 19, 2016

  CHAMBUA: YANGA WAKIKUBALI KUANZA KUFUNGWA WAMEKWISHA!

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Sekilojo Johnson Chambua amewashauri wachezaji wa Yanga kucheza kwa makini leo dhidi ya APR wasiwaruhusu kutangulia kupata bao.  
  Yanga wanawakaribisha APR ya Rwanda jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya wiki iliyopita kushinda 2-1 mjini Kigali.
  Na Chambua kiungo mshambuliaji hodari wa zamani wa Yanga, ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE kwamba; “Ni kosa kubwa Yanga kuwaruhusu APR kutangulia kupata bao, na ninadhani huo ndiyo utakuwa mpango wa APR, kuja kutafuta bao la mapema,”amesema.
  Sekilojo Chambua (kulia) enzi zake anawika Taifa Stars na Yanga. Kushoto ni Edibily Jonas Lunyamila waliyewika naye Yanga pia  
  “Safu ya ulinzi ya Yanga imekuwa ikiruhusu mabao yasiyotarajiwa wakati fulani, leo wanapaswa kuwa makini mno, wahakikishe APR hawawatangulii na kwa ujumla wasiwaruhusu kabisa kupata bao leo,”amesema Chambua.
  Sare yoyote ni nzuri kwa Yanga na watasonga hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ikitokea bahati mbaya ya kufungwa 1-0 pia watafuzu.
  Wakifungwa 2-1 mchezo utahamia kwenye mikwaju ya penalti, lakini wakifungwa 3-2 watatolewa kwa mabao ya ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa 4-4, lakini APR watasonga mbele kwa kufunga mabao mengi ugenini.
  Na Yanga leo itamkosa beki wake aliye katika kiwango kizuri kwa sasa, Juma Abdul Jaffar ambaye atakuwa anatumikia adhabu ya kadi za njano mfululizo 
  Mfungaji huyo wa bao la kwanza katika ushindi wa 2-1 dhidi ya APR Jumamosi iliyopita mjini Kigali, alipewa kadi katika mechi mbili mfululizo zilizopita dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius na APR.
  Na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm hana shaka kwa sababu Mkongomani Mbuyu Twite ataziba pengo la Juma Abdul dhidi ya timu yake ya zamani.
  Mshindi wa jumla atakiutana na mshindi kati ya Al Ahly ya Misri na Recreativo de Libolo ya Angola katika 16 Bora. 
  Viingilio vya mchezo wa leo ni Sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya Chungwa, Bluu na Kijani, Sh. 25,000 kwa VIP A na 20,000 kwa VIP B na C – tiketi zimeanza kuuzwa mapema leo katika maeneo ya siku zote, ikiwemo Uwanja wa karume na Uwanja wa Taifa. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CHAMBUA: YANGA WAKIKUBALI KUANZA KUFUNGWA WAMEKWISHA! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top