• HABARI MPYA

  Thursday, March 17, 2016

  APR WAIFUATA YANGA DAR KIVINGINE

  Na Augustin Bigirimana, KIGALI
  APR ya Rwanda inaondoka leo saa 7:00 mchana mjini Kigali, Rwanda kuja Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa marudiano Raundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Yanga SC Jumamosi na kocha Mtunisia, Nizar Khanfir amepania kushinda ugenini.
  Licha ya kufungwa mabao 2-1 Jumamosi Uwanja wa Amahoro, Kigali kocha huyo anayeingia katika wiki yake ya pili kazini, ameonekana wazi kupania kuigeuzia kibao Yanga.
  APR ilifanya mazoezi yake ya mwisho jana viwanja vya Kicukiro na bahati nzuri kwao ni kwamba, mshambuliaji wake hatari, Issa Bigirimana aliyekosa mchezo wa kwanza amerudi.
  APR wanataka kuigeuzia kibao Yanga Dar es Salaam

  Bigirimana aliyekosa mchezo huo kutokana na kuwa kwenye msiba wa mama yake mzazi, jana amefanya mazoezi kikamilifu na wenzake na atasafiri na timu kuja Dar.
  Bahati mbaya kwao APR, beki Ngabo Albert ataendelea kuwa nje kwa sababu ya maumivu sawa na mshambuliaji Michel Ndahinduka anayesumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
  Kocha Nizar Khanfir aliwaambia Waandishi wa Habari jana kwamba anataka kuimarisha safu yake ya ushambuliaji kwa kumuanzisha Bigirimana Jumamosi Uwanja wa Taifa.
  Na kwa ujumla kocha huyo anatarajiwa kufanya mabadiliko mawili kutoka kikosi cha mechi ya kwanza, Bigirimana akichukua nafasi ya Mubumbyi na Benedata akichukua nafasi ya mpwa wa kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, Djihad.
  Wenyeji Yanga pamoja na kuonekana kutoupa uzito mchezo huo wakiweka kambi katika hoteli ya hadhi ya chini Kariakoo, lakini Kocha Mholanzi Hans van der Pluijm amesema wanajiandaa kwa mazoezi ya kutosha.
  Pluijm alisema licha ya kupata ushindi wa mabao 2-1 ugenini mjini Kigali, lakini anataka washinde na nyumbani pia.
  "Tunaendelea kurekebisha baadhi ya makosa, katika soka kila siku unajifunza kitu kipya. Kikubwa kwetu ni maandalizi ili kushinda kila mechi tunayocheza,”amesema.
  Yanga nayo itawakosa wachezaji wake watatu Jumamosi, kiungo Said Juma 'Makapu' na  mshambuliaji Matheo Anthony, ambao wameshindwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi uliopo barabara ya Kilwa, Dar es Salaam kutokana na kusumbuliwa na Malaria.
  Yanga pia itaendelea kumkosa Nahodha wake, Nadir Haroub 'Cannavaro' ambaye ni majeruhi wa muda mrefu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: APR WAIFUATA YANGA DAR KIVINGINE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top