• HABARI MPYA

    Sunday, November 24, 2019

    STARS YAPANGWA KUNDI C KOMBE LA CHALLENGE NA MABINGWA WATETEZI, KENYA NA ZANZIBAR

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TANZANIA Bara ‘Kilimanjaro Stars’ wamepangwa Kundi C kwenye KOmbe la Mataifa yaAfrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge inayotaraiwa kuanza Desemba 7 hadi 19 mjini Kampala nchini Uganda.
    Kilimanjaro Stars, mabingwa wa 1975, 1994 na 2010 wamepangwa pamoja na ndugu zao, Zanzibar ‘Heroes’, Djibouti na mabingwa watetezi, Kenya ‘Harambee Stars’.
    Kundi A linaundwa na wenyeji, Uganda, Burundi, Ethiopia na Eritrea, wakati Kundi B linaundwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Sudan, Sudan Kusini na Somalia.

    Timu mbili za juu kutoka kila kundi zitaingia Robo Fainali zikiungana na mbili nyingine zitakazomaliza na wastani mzuri katika nafasi ya tatu. 
    CECAFA Challenge ndiyo michuano mikongwe zaidi ya soka barani Afrika ambayo ilianza mwaka 1926 ikijulikana kama Kombe la Gossage hadi mwaka 1966, ilipobadilishwa na kuwa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati hadi mwaka 1971 ilipobadilishwa tena na kuwa CECAFA Challenge.
    Uganda ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo tangu mwaka 1971, wakiwa wamelitwaa mara 14, wakifuatiwa na Kenya mara saba, Ethiopia mara nne na Tanzania mara tatu.
    Mara ya mwisho Tanzania Bara ilitwaa Kombe hilo mwaka 2010 mjini Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha Mdenmark, Jan Borge Poulsen.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS YAPANGWA KUNDI C KOMBE LA CHALLENGE NA MABINGWA WATETEZI, KENYA NA ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top