• HABARI MPYA

    Monday, November 25, 2019

    KENYA WATWAA KOMBE LA CECAFA CHALLENGE BAADA YA KUIPIGA TANZANIA BARA 2-0 CHAMAZI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KENYA imefanikiwa kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati kwa Wanawake, CECAFA Challenge baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
    Ushindi huo ni sawa na kulipa kisasi baada ya Kenya kufungwa na Tanzania Bara 4-1 katika fainali mwaka 2016 nchini Uganda.
    Tanzania Bara ndio waliokuwa mabingwa watetezi, baada ya kutwaa taji mwaka jana mjini Kigali nchini Rwanda wakiizidi Kenya kwa wastani wa mabao baada ya kulingana kwa pointi katika michuano iliyocheza kwa mfumo wa Ligi. 
    Katika mchezo wa leo, shujaa wa Kenya amekuwa mshambuliaji wake chipukizi, Jentrix Shikangwa aliyefunga mabao yote hayo kipindi cha pili baada ya kutokea benchi kama ilivyo kawaida yake.


    Shikangwa ambaye ameibuka mfungaji bora kwa mabao yake 10, alifunga bao la kwanza kwa penalti dakika ya 71 baada ya Deonisia Minja kuushika mpira akijaribu kuokoa na la pili akafunga kwa shuti la umbali wa mita 20 dakika ya 88.
    Baada ya bao la pili kipa wa Tanzania hakuinuka na akatolewa nje kwa machela nafasi yake ikichukuliwa na Zubeda Mgunda aliyekwenda kumalizia vizuri mechi hiyo.
    Kilimanjaro Queens ilijifariji kwa tuzo ya Timu yenye Nidhamu, huku mchezaji wake, Mwanahamisi Omary Shaluwa ‘Gaucho’ akishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano na kipa Bora ni Annedy Kundu wa Kenya. 
    Uganda ilifanikiwa kumaliza nafasi ya tatu baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Burundi, mabao ya Amina Nabibi dakika ya 64 na Shamira Nalujja dakika ya 84 hapo hapo Azam Complex.
    Kikosi cha Tanzania Bara kilikuwa; Naijat Idrisa, Happyness Mwaipaja, Amina Bilal, Deonisia Minja, Mwanahamisi Omary ‘Gaucho’, Anastazia Katunzi/Stumai Abdallah, Julitha Singano, Fatuma Salum, Asha Rashid ‘Mwalala’/Opa Sanga, Enekia Kasongo na Asha Shaaban. 
    Kenya; Annedy Kundu, Mwanalima Jereko, Nelly Sawe, Janet Bundi/Jentrix Shikangwa, Mercy Airo, Dorcus Nixon, Sheryl Andiba, Ruth Ingosi/Situma Topister, Cynthia Musungu, Vivien Makokha na Corazone Aquinho.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KENYA WATWAA KOMBE LA CECAFA CHALLENGE BAADA YA KUIPIGA TANZANIA BARA 2-0 CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top