• HABARI MPYA

    Saturday, November 23, 2019

    MIRAJ ATHUMANI ‘MADENGE’ APIGA MBILI SIMBA SC YAITANDIKA RUVU SHOOTING MABAO 3-0

    Na Mwandshi Wetu, DAR ES SALAAM
    MABINGWA watetezi, Simba SC leo wameiadhibu Ruvu Shooting baada ya kuichapa mabao 3-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
    Nyota wa mchezo wa leo alikuwa ni mshambuliaji Miraji Athumani ‘Madenge’ aliyefunga mabao mawili, huku linguine likifungwa na beki Mbrazil, Tairone Santos da Silva.
    Na kwa ushindi huo, Wekundu wa Msimbazi wanafikisha pointi 25 katika mchezo wa 10 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu ikifuatiwa na Kagera Sugar yenye pointi 23 za mechi 11, wakati Ruvu Shooting inabaki pointi zake 15 baada ya kucheza mechi 12.


    Miraj anayefahamika pia kwa jina la utani Sheva akifananishwa na mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Ukraine, Andriy Mykolayovych Shevchenko alifunga bao la kwanza dakika ya 39 kwa kichwa akimalizia krosi ya beki wa kulia Shomari Kapombe.
    Beki Mbrazil, Tairone Santos da Silva aliye katika msimu wake wa kwanza tangu asajiliwe kutoka Atletico Cearense ya Daraja la Nne nchini kwao akafunga bao la pili dakika ya 47 akimalizia mpira wa kona wa kiungo Mkenya, Francis Kahata kutoka kulia.
    Miraj aliyeibukia timu ya vijana ya Simba, maarufu kama Simba B kabla ya kwenda kujikomaza kisoka Mwadui FC ya Shinyanga, Toto African ya Mwanza na Lipuli FC ya Iringa kisha kurejea nyumbani msimu huu, alifunga bao la tatu kwa shuti dakika ya 74 akimalizia pasi ya mshambuliaji mwenzake, Mnyarwanda Meddie Kagere.
    Kikosi cha Ruvu Shooting kilikuwa; Mohamed Makaka, Omary Kindamba, Kassim Simbaulanga, Renatus Ambroce, Rajab Zahir, Zuberi Dabi, Emmanuel Martin, Shaaban Msala/Moses Shaaban dk73, Saadat Mohamed, Said Dilunga/Fully Maganga dk58 na Edward Christopher/Abdulrahman Mussa dk61.
    Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Tairone Santos, Pascal Wawa, Gerson Fraga ‘Viera’, Hassan Dilunga/Deo Kanda dk63, Muzamil Yassin, Meddie Kagere/Ibrahim Ajibu dk75, Miraji Athuman ‘Madenge’ na Francis Kahata/Sharaff Eldin Shiboub dk79.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MIRAJ ATHUMANI ‘MADENGE’ APIGA MBILI SIMBA SC YAITANDIKA RUVU SHOOTING MABAO 3-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top