• HABARI MPYA

    Wednesday, November 20, 2019

    KAMA SAMATTA ANACHEZA VIBAYA, NI NANI ALIYECHEZA VIZURI STARS?

    Na Gift Macha, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI Mbwana Samatta ndiye staa wa Tanzania kwenye soka. Ndiye mchezaji bora zaidi kuwahi kutokea Tanzania. Hili halina ubishi.
    Kwenye kikosi cha Taifa Stars ndiye mchezaji aliyepiga hatua zaidi. Ndiye mchezaji aliyefanikiwa zaidi. Ndiye mchezaji mwenye kipaji zaidi. Kuna mtu anayebisha? Basi atakuwa na chuki binafsi.  
    Siku zote tumekuwa tukimtazama Samatta kama kioo cha soka letu. Tumekuwa tukimtazama kama Mkombozi wetu. Hata hivyo bado kuna maswali mengi juu ya namna Samatta anavyowajibika kwenye timu ya Taifa. 
    Kuna ambao wanasema Samatta hana msaada na timu. Kuna ambao wanasema Samatta ni muhimu. Mjadala ni wa moto kweli kweli. 
    Hata hivyo naomba tulitazame hili kwa makini. Mjadala huu uanze kwenye takwimu, kisha tutarejea uwanjani. Katika michezo nane ya mwisho ya Taifa Stars ambayo Samatta amecheza, amefunga mabao matano na kutoa pasi tatu za mabao. Mechi nyingine moja aliangushwa ikazaliwa penalti, ilikuwa dhidi ya Uganda. 
    Mgawanyo wa mabao yake kuanzia Oktoba mwaka jana uko kama hivi. Aliwafunga Cape Verde bao moja na kutoa pasi ya bao la pili wakati Tanzania ikishinda 2-0 jijini Dar. Alitoa pasi nyingine ya bao na kufanyiwa faulo iliyozaa penalti kwenye ushindi wa 3-0 dhidi ya Uganda mapema mwaka huu. Samatta akafunga bao jingine na kutoa pasi ya bao kwenye mechi ya AFCON dhidi ya Kenya pale Misri.
    Baada ya AFCON ameichezea Taifa Stars mechi nne na kufunga mabao mawili. Alifunga kwenye mechi ya kuwania kufuzu hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya Kombe la Dunia dhidi ya Burundi. Amefunga tena jana usiku dhidi ya Libya, kwa mkwaju wa penalti. 
    Ni Saimon Msuva pekee aliyeweza kufunga idadi hiyo ya mabao. Msuva amefunga mara tano kama Samatta, lakini nusu ya magoli yake yalitokana na pasi kutoka kwa Samatta. Kwa kifupi, Msuva ameng’ara kwenye michezo hiyo kutokana na msaada mkubwa anaopewa na Mbwana.
    Mechi ambazo Msuva amefunga kwenye kipindi cha mwaka mmoja uliopita ni dhidi ya Cape Verde, Uganda, Kenya, Burundi na Equatoria Guinea. Inavutia sana. Je Samatta anang’ara kwa msaada wa nani?
    Turejee Uwanjani sasa. Ni kweli kwamba kwa siku za karibuni, Samatta amepungua nguvu kidogo katika timu ya Taifa. Wengi tunatamani kuona akifanya kile alichokifanya dhidi ya Liverpool pale Anfield. Wengi tunatamani kuona akifanya zaidi na zaidi, lakini tumewahi kujiuliza, nani anamsaidia Samatta kufanya hayo?
    Kwenye kikosi cha Stars, washambuliaji wengine wote wanamtegemea Samatta. Wanasubiri yeye apige chenga kisha awape pasi za kufunga. Ni nani ambaye anacheza kwaajili ya Samatta? Nani amewahi kupiga chenga na kumtengenezea Samatta nafasi za wazi katika mechi za Stars? 
    Kabla hatujamlaumu Samatta, tujiulize ni kwa kiasi gani timu inacheza kwaajili yake. Ni lazima tujiulize ni mchezaji gani anajituma ili Samatta aweze kung’ara katika kikosi cha Stars? Bila shaka hakuna. 
    Tunamtaka Samatta awe Mungu mtu. Tunataka akabe, apige chenga, atoe pasi za mabao na akafunge mwenyewe. Duniani kote hii haipo. Inatokea mara chache sana. Lazima timu ifanye kitu kwaajili ya Samatta, ili aweze kung’ara na kuisaidia timu.
    Nadhani wakati huu ambao tuna mechi muhimu za kuwania kufuzu AFCON na Kombe la Dunia, tunamuhitaji Samatta akiwa bora zaidi. Tunahitaji kumtia moyo zaidi. Wachezaji wenzie wanahitaji kufahamu kuwa ipo haja ya kucheza kwaajili ya Samatta. Nadhani hapa tutakuwa tunajenga.
    Nyakati za sasa siyo za kunyoosheana vidole, ni nyakati za kushikamana. Tukianza kumlaumu Samatta kwa kutocheza kwenye ubora wa juu hatutakuwa salama. Kama Samatta anacheza vibaya, tumtaje aliyecheza vizuri. Wengine wamefanya kitu gani cha ajabu?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMA SAMATTA ANACHEZA VIBAYA, NI NANI ALIYECHEZA VIZURI STARS? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top