• HABARI MPYA

  Monday, February 11, 2019

  WAMBURA APELEKWA RUMANDE BAADA YA KUSOMEWA MASHITAKA 17 LEO KISUTU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MAKAMU wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Richard Wambura amepelekwa rumande baada ya kunyimwa dhamana kufuatia kusomewa mashitaka 17, yakiwemo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha zaidi ya Sh. Milioni 100.
  Wambura, aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mara (FAM), alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mjini Dar es Salaam  leo kufuatia kushikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa siku tatu.
  Wambura aliyewahi pia kuongoza klabu ya Simba na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), amepelekwa rumande baada ya kusomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina na Wakili wa Serikali, George Barasa, akidaiwa kutenda makosa hayo katika ofisi za TFF kati ya Julai mwaka 2004 na mwaka 2015.
  Michael Wambura amepelekwa rumande leo baada ya kunyimwa dhamana kufuatia kusomewa mashitaka 17 Mahakama ya Kisutu

  Barasa amedai Julai 7 mwaka 2004, Wambura alipeleka barua ya kughushi TFF akijifanya imeandikwa na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Jek System Limited ikidai malipo ya mkopo wa dola za Kimarekani 30,000 zilizokopwa na shirikisho hilo pamoja na riba.
  Wambura anadaiwa kujipatia fedha hizo kwa wakati tofauti na anashitakiwa kwa mashtaka mawili ya kutakatisha fedha, kwanza kati ya Agosti 15 na Oktoba 24 alitakatisha Sh. 25,050,000 na 75,945,024 huku akijua fedha hizo ni zao la kosa la kughushi.
  Amenyimwa dhamana na kupelekewa rumande hadi Februari 14, mwaka huu kesi hiyo itakapoendelea hapo hapo Mahakama ya Kisutu.
  Mapema leo, kupitia kwa Mwanasheria wake, Emmanuel Muga Wambura alitangaza kujitoa kwenye mambo ya michezo na kujivua nyadhifa zote ikiwa pamoja na kufuta kesi aliyoifungua Mahakama Kuu dhidi ya TFF.
  Wambura anakuwa kiongozi mwingine mkubwa wa zamani wa TFF kushikiliwa na dola kwa makosa ya ubadhirifu, baada ya aliyekuwa Rais, Jamal Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa ambao wapo rumande tangu Julai mwaka juzi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAMBURA APELEKWA RUMANDE BAADA YA KUSOMEWA MASHITAKA 17 LEO KISUTU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top