• HABARI MPYA

  Monday, February 11, 2019

  AZAM FC YASAWAZISHA BADO DAKIKA TISA KUPATA SARE YA 1-1 NA LIPULI NA IRINGA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Azam FC imelazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Lipuli Uwanja wa Samora mjini Iringa katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara. 
  Katika mchezo huo uliokuwa mkali na wa kusisimua, Lipuli FC waliotangulia kwa bao la Daruwesh Saliboko dakika ya 45 na ushei, kabla ya Azam FC kusawazisha kupitia kwa kiungo wake, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dakika ya 81. 
  Kwa sare hiyo ya pili mfululizo, Azam FC inafikisha pointi 49, baada ya kucheza mechi 22, sasa inazidiwa pointi tisa na vinara Yanga SC ambao hata hivyo wamecheza mechi moja zaidi, wakati Lipuli inapanda kwa nafasi moja hadi ya nne ikifikisha pointi 37 katika mechi ya 25.
  Salum Abubakar 'Sure Boy' (kulia) ameisawazishia Azam FC zikiwa zimebaki dakika tisa mchezo kumalizika
  Beki wa Lipuli, Novaty Lufunga akimchezea rafumshambuliaji Mzambia wa Azam FC, Obrey Chirwa

  Lipuli FC inayofundishwa na kiungo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Suleiman Abdallah Matola, sasa inawazidi kwa pointi moja mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 36 lakini za mechi 15.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, mabao ya Yusuf Mhilu dakika ya 40 na Mohamed Mkopi dakika ya 64 yamewapa wenyeji, Ndanda FC ushindi wa 2-0 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
  Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, bao pekee la Raizin Hafidh dakika ya 60 limewapa wageni Coastal Union ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbao FC, huku Tanzania Prisons ikiendelea kufanya vizuri chini ya kocha mpya, Mohammed ‘Adolph’ Rishard baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Stand United, bao pekee la Adam Adam dakika ya 51 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Wenyeji Mwadui FC wakaibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga, bao pekee la Salim Aiyee dakika ya 75, wakati African Lyon imelazimishwa sare ya 0-0 na Ruvu shooting Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YASAWAZISHA BADO DAKIKA TISA KUPATA SARE YA 1-1 NA LIPULI NA IRINGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top