• HABARI MPYA

  Sunday, June 17, 2018

  TARIMBA: KAMATI YANGU INAFANYA MAMBO KIMYA KIMYA YANGA, YAKIKAMILIKA TUTAIBUKA KWA KISHINDO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Kusimamia Shughuli mbalimbali za Yanga kwa wakati huu, Tarimba Abbas amesema kwamba wanafanya mambo yao kwa siri ili kuepuka kuwapa faida wapinzani wao.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari jana mjini Dar es Salaam, Tarimba amesema kwamba wanafanya shughuli zao kimya kimya ikiwemo usajili na mara mambo yote yatakapokamilika wataweza hadharani.
  “Kamati yetu imepewa majukumu maalum na mkutano mkuu wa Yanga uliofanyika Jumapili iliyopita, Sasa kikubwa ambacho ningependa labda niwaambie wana Yanga, katika kipindi ambacho Kamati itakuwa inafanya kazi yake, kwanza tutakuwa tunamfukuza mwizi kimya kimya,”alisema Tarimba na kuongeza. “Hatutakuwa na kutangaza mara kwa mara miamala ambayo tunafanya. Miamala yetu sote sisi itakuwa ni siri yetu sisi na Kamati ya Utendaji na vile vile tukishirikiana na Kamati ya Usajili, sasa ningeomba tu Watanzania, haswa wapenzi wa Yanga, wakae kimya wasubiri kazi ambayo sisi tumepewa tutaifanya kwa uadilifu na kwa mapenzi ya hali ya juu na wasiwe na wasiwasi,”
  Tarimba Abbas amesema kwamba wanafanya mambo yao kwa siri ili kuepuka kuwapa faida wapinzani wao

  Pamoja na kukubaliana kwa kauli moja kumrejesha madarakani, Mwenyekiti wao Yussuf Mehboob Manji katika mkutano Mkuu wa mwaka uliofanyika Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam Juni 10, wanachama wa Yanga pia waliunda Kamati ya watu tisa chini ya Rais wa zamani wa klabu, Tarimba Abbas na Makamu wake, Saidy Meckysadik, kusimamia usajili na mambo mengine muhimu ya klabu kwa sasa.
  Wajumbe wa Kamati hiyo ni Abdallah Bin Kleb, Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Lucas Mashauri, Yusuphed Mhandeni, Hamad Islam, Makaga Yanga, Ridhiwani Kikwete, Majjid Suleiman na Hussein Ndama.
  Yanga SC imekuwa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti tangu Mei mwaka jana kufuatia kujiuzulu kwa Mwenyekiti, Manji.
  Lakini idadi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka uongozi wa Manji uliochaguliwa Juni mwaka 2016 imepungua pia baada ya kujizulu kwa Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.  Waliobaki katika Kamati ya Utendaji pamoja na Sanga ni Wajumbe watatu, Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala na Hussein Nyika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TARIMBA: KAMATI YANGU INAFANYA MAMBO KIMYA KIMYA YANGA, YAKIKAMILIKA TUTAIBUKA KWA KISHINDO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top