• HABARI MPYA

    Sunday, June 17, 2018

    WANA YANGA WANATAKA KUSIKIA KAULI MOJA TU YA MANJI KUHUSU MAAZIMIO YA MKUTANO WA JUNI 10

    JUNI 10, mwaka huu, yaani mwishoni mwa wiki iliyopita, wanachama wa klabu ya Yanga walikubaliana kwa kauli moja kumrejesha madarakani, Mwenyekiti wao Yussuf Mehboob Manji katika mkutano Mkuu wa mwaka uliofanyika Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.
    Pamoja na kumrejesha Maji aliyejiuzulu Mei mwaka jana, wanachama hao waliunda Kamati ya watu tisa chini ya Rais wa zamani wa klabu, Tarimba Abbas na Makamu wake, Saidy Meckysadik, kusimamia usajili na mambo mengine muhimu ya klabu kwa sasa.
    Wajumbe wa Kamati hiyo ni Abdallah Bin Kleb, Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Lucas Mashauri, Yusuphed Mhandeni, Hamad Islam, Makaga Yanga, Ridhiwani Kikwete, Majjid Suleiman na Hussein Ndama.

    Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya mkutano huo Jumapili ya wiki iliyopita, Kaimu Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa alisema kwamba agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harison Mwakyembe kufanyika kwa uchaguzi wa kuziba nafasi za viongozi waliojiuzulu ndani ya miezi miwili pia linafanyiwa kazi.
    Mkwasa pia alisema kwamba wameridhia mwongozo wa mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu kwa kuingia kwenye soko la hisa na kwamba mchakato wa zoezi hilo unashughulikiwa na Wakili maarufu, Alex Mgongolwa. 
    Mapema akifungua mkutano huo, Waziri Mwakyembe pamoja na kuipongeza Yanga kwa klabu yenye mafanikio makubwa nchini, pia aliwapa miezi wawe wamefanya uchaguzi ili kuziba mapengo ya viongozi walioondoka.
    Waziri Mwakyembe alisema Yanga inahitaji kuwa na uongozi imara utakaosajili wachezaji wazuri wa kuirejeshea heshima klabu kwa kufanya vizuri kwenye mashindano. “Mkifanikiwa Yanga, nimefanikiwa mimi kama Serikali...mnatakiwa kupata kundi la wanachama ambao mtasaidiana kuvuka katika kipindi hiki cha mpito,”alisema.
    Aidha, Mwakyembe aliwataka wale wanaopinga mabadiliko ya mfumo wa uendeshwa wa klabu hiyo kufika kwenye mkutano kutoa ya moyoni na wakishindwa wamfuate ofisini kwake.
    Pamoja na Waziri Mwakyembe, Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Huruma Mkuchika ambao walianza kwa kikao cha faragha na uongozi wa Yanga chini ya Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga.
    Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Singo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya, Jaji John Mkwawa na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu pamoja na Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa.
    Manji aliingia Yanga mwaka 2006 kama mdhamini kupitia kampuni yake ya Lotto Kitita, lakini baadaye akawa mfadhili Mkuu wa klabu kabla ya kuwa Mwenyekiti.
    Katika kipindi chake cha kuwa mfadhili na Mwenyekiti wa Yanga, Manji aliifanyia mengi klabu– kubwa ni kuirejeshea hadhi na heshima klabu hiyo.
    Alipoingia mwaka 2006 aliikuta klabu ipo dhoofu kiuchumi na haiwezi kushindana na mahasimu wao, Simba katika kuwania wachezaji bora ambao ndiyo mtaji wa kushinda mataji.
    Wakati huo Yanga ilikuwa inasajili wachezaji ambao ama walikuwa wameachwa na timu zao, waliojipeleka wenyewe kwa mapenzi yao au waliopatikana kwa njia ya mchujo wa majaribio.
    Lakini mara baada ya Manji kuingia Yanga, klabu hiyo ikaanza kusifika kwa kusajili wachezaji wa kigeni na wale nyota wa hapa nyumbani, ikiwa ni pamoja na kubomoa ngome ya mahasimu, Simba SC.
    Mwaka 2009 fedha za Manji zilimtoa kipa kipenzi cha wana Simba Msimbazi, Juma Kaseja na desturi hiyo ikaendelea baadaye wakichukuliwa beki Kelvin Yondan na mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi.
    Yanga iliipiku Simba ‘kimafia’ katika kumsajili beki anayeweza kucheza kama kiungo pia, Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda, tu kwa jeuri ya fedha.
    Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alianza kuonekana akimsainisha Mbuyu mjini Kigali, lakini baadaye Mwenyekiti wa Usajili wa timu ya Jangwani, Abdallah Bin Kleb akaingia kwa ‘gia kubwa’ na kubadilisha mambo, Mbuyu akatua Jangwani.
    Na ni katika kipindi hicho imeshuhudiwa Manji amewazima kabisa Simba na Yanga ikitawala soka ya Tanzania na kuzidi kujiongezea mashabiki na wapenzi.
    Lakini migogoro haikukosekana pia wakati wa utawala wa Manji, ambayo wakati fulani iliiathiri timu mfano ule wa kutaka kumng’oa aliyekuwa Mwenyekiti, Wakili Lloyd Nchunga ulioiponza klabu ifungwe 5-0 na mahasimu, Simba Mei 6, mwaka 2012.
    Mapema mwaka jana, Manji alikuja na mpango wa kutaka kujikodisha klabu kupitia kampuni aliyoisajili kwa jina la Yanga Yetu, lakini ukapata upinzani mkali na kuamua kuachana nao.  
    Kabla ya kufikia maamuzi haya, Manji alipitia kwenye misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Aprili, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na baadaye akidaiwa kumiliki pasipoti mbili.
    Kwa sasa klabu inakabiliwa na hali ngumu kiuchumi kiasi cha kuambulia ushindi wa mechi moja kati ya 14 zilizopita, nyingine saba wakifungwa na sita kutoa sare. Na wana Yanga wako tayari Manji arejee kwa sharti lolote kuinusuru klabu.
    Na baada ya mkutano wa wiki iliyopita kitu kizuri ambacho wana Yanga watapenda kusikia ni kauli ya kipenzi chao, Manji kwanza tu kujibu azimio lao, ingawa aina ya jibu pia nalo ni suala lingine.
    Hadi sasa wana Yanga wapo njia panda, maana hawajui nini haswa mustakabali wa klabu yao na msimamo wa Mwenyekiti wao kipenzi, Manji kama atakubali ombi lao au la.
    Kwa sasa wana Yanga kwanza wanahitaji kujua msimamo wa kipenzi chao Manji, je yu tayari kurudi ili watulie wakijua mwelekeo wa klabu yao – lakini pia hata kama hataweza kurudi, itawasaidia kujua kwamba hawajapata suluhisho la matatizo ya klabu yao.
    Na hapo ndipo utakapoonekana umuhimu wa uongozi kuchukua hatua zaidi na za haraka katika kutafuta suluhisho la matatizo ya klabu na kwa kuwa, Waziri Mwakyembe amekwishatoa agizo klabu ifanye uchaguzi wa kujaza nafasi zilizo wazi za watu walioondoka, bila shaka huo utakuwa mwanzo wa klabu kupata kiongozi mpya mkuu.
    Na ndiyo maana mimi Mahmoud Ramadhani Bin Zubeiry leo nikiwa Jijini Washington, Marekani natumia nafasi yangu hii kumuomba Manji popote alipo ainuke na kuwajibu wana Yanga juu ya maazimio ya Mkutano wa Juni 10, pale Bwalo la Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WANA YANGA WANATAKA KUSIKIA KAULI MOJA TU YA MANJI KUHUSU MAAZIMIO YA MKUTANO WA JUNI 10 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top