• HABARI MPYA

  Saturday, June 02, 2018

  SINGIDA UNITED YAJIFARIJI KWA KUMSAJILI KIYOMBO NA KUMTAMBULISHA MOROCCO MRITHI WA PLUIJM

  Na Mwandishi Wetu, ARUSHA
  MARA tu baada ya kuchapwa mabao 3-2 na Mtibwa Sugar katika fainali ya Komba la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC), Singida United imejifariji kwa kumtambulisha mshambuliaji mpya, Habib Hajji Kiyombo na kocha mpya, Hemed Suleiman Ali ‘Morocco’.
  Mkurugenzi wa Singida United, Sanga Festo alijitutumua na kusahau machungu ya kipigo na kukosa Kombe la TFF kwa kwenda kuwatambulisha Kiyombo kutoka Mbao FC na Morocco ambaye alikuwa kocha wa kikosi cha Zanzibar kilichofika fainali ya Kombe la CECAFA Challenge mwaka jana nchini Kenya.
  Sanga Festo amesema kwamba Kiyombo amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na timu hiyo ambayo inaingia kwenye msimu wake wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara tangu ipande.

  Mkurugenzi wa Singida United, Sanga Festo akipeana mikono na Habib Kiyombo baada ya kumsajili hivi karibuni kabla ya kumtambulisha leo

  Morocco anachukua nafasi ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ambaye tayari amesaini mkataba wa kujiunga na Azam FC kaunzia msimu yao – hiyo ikiwa timu yake ya tatu nchini baada ya awali kufundisha Yanga SC.
  Pluijm ameaga kwa majonzi leo, akishindwa kuipa Singida United taji la ASFC kufuatia kipigo cha 3-2 kutoka kwa Mtibwa Sugar mjini Arusha.
  Shujaa wa Mtibwa Sugar leo alikuwa ni kiungo Ismail Mhesa aliyefunga bao la tatu na la ushindi dakika ya 88 na kuamsha shangwe za mashabiki wa timu hiyo kutoka Manungu mkoani Morogoro.
  Na hiyo ilikuwa ni baada ya Singida United kutoka nyuma kwa 2-0 na kusawazisha mabao yote na kuwa 2-2 kiasi cha kupata nguvu zaidi na kuanza kutawala mchezo.
  Na Mhesa aliifungia Mtibwa Sugar bao la ushindi dakika 10 tu tangu waanze kucheza pungufu, kufuatia beki wao wa kushoto Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ kutolewa kwa kadi nyekundu ya utata na refa Emmanuel Mwandemwa wa hapa, aliyekuwa anasaidiwa na Mohammed Mkono wa Tanga Ferdinand Chacha wa Mwanza.
  Mtibwa Sugar ya kocha Zuberi Katwila iliuanza vizuri mchezo huo na kufanikiwa kuongoza kwa 2-0 kwa mabao ya Salum Kihimbwa dakika ya 22 na Baba Ubaya dakika ya 37 kabla ya kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 78.
  Dakika mbili kabla ya mapumziko, Singida United walizinduka na kupata bao la kwanza lililofungwa na Salum Chuku na timu hizo zikaenda kupumzika matokeo yakiwa 2-1.
  Kipindi cha pili Singida United waliokuwa wanacheza kwa mara ya mwisho chini ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm ambaye anahamia Azam FC waliingia kwa kasi na kusukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa Mtibwa Sugar.
  Na haikuwa ajabu Singida United walipofanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 69 kupitia kwa kiungo wake mshambuliaji, Tafadzwa Kutinyu – kabla ya Mhesa kupeleka Kombe la TFF Manungu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SINGIDA UNITED YAJIFARIJI KWA KUMSAJILI KIYOMBO NA KUMTAMBULISHA MOROCCO MRITHI WA PLUIJM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top