• HABARI MPYA

  Sunday, April 01, 2018

  SINGIDA UNITED WAIFUATA JKT TANZANIA NUSU FAINALI AZAM SPORTS FEDERATION

  Na Prince Akbar, SINGIDA
  TIMU ya Singida United imefanikiwa kuingia Nusu Fainali ya michuano ya Azam Sports Federation Cup kwa ushindi wa penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.
  Kiungo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Papy Kabamba Tshishimbi alipiga juu ya lango penalti ya kwanza ya Yanga na winga Emmanuel Martin akagongesha mwamba wa chini kulia mkwaju wake, wakati waliofunga penalti za wana Jangwani hao ni Nahodha Kelvin Yondan na Gardiel Michael.
  Kipa wa Yanga, Mcameroon Youthe Rostand alipangua vizuri mkwaju wa Malik Antil lakini akashindwa kuokoa mashuti ya Shafiq Batambuze, Tafadzwa Kutinyu, Kenny Ally na Elinyeswia Sumbi ‘Msingida’.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa Hans Mabena kutoka Tanga aliyeasaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Jesse Erasmo wa Morogoro, hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lilifungwa na kinda Yussuf Mhilu, tunda la timu ya vijana ya klabu hiyo, dakika ya 23 kwa kichwa akitumia udhaifu wa beki wa Singida Kennedy Juma Wilson kumalizia kona ya Ibrahim Ajib kutoka upande wa kulia.
  Lakini mwanzoni tu mwa kipindi cha pili, dakika ya 46 ya mchezo Singida United wakasawazisha bao hilo kupitia kwa kiungo Kenny Ally Mwambungu aliyepenyezewa pasi nzuri na Mudathir Yahya aliyetumia udhaifu wa wachezaji wa Yanga kuzubaa.
  Singida United sasa itakutana na JKT Tanzania iliyorejea Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuelekea msimu ujao, ambayo jana iliwafunga wenyeji, Tanzania Prisons 2-0 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. 
  Nusu Fainali nyingine ya Azam Sports Federation itazikutanisha Mtibwa Sugar iliyoitoa Azam FC kwa penalty 9-8 baada ya sare ya 0-0 na Stand United iliyoichapa Njombe Mji FC 1-0. Juzi mjini Shinyanga. 
  Kikosi cha Singida United kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Michael Rusheshangoga, Shafiq Batambuze, Juma Kennedy, Malik Antiri, Mudathir Yahya, Nizar Khalfan, Kenny Ally, Lubinda Mundia, Tafadzwa Kutinyu na Kiggy Makassy/Elinyeswia Sumbi dk90+2.
  Yanga SC; Youthe Rostand, Juma Abdul/Hassan Kessy dk83, Gardiel Michael, Andrew Vincent, Kelvin Yondan, Said Juma ‘Makapu’/Emmanuel Martin dk65, Yussuf Mhilu, Papy Kabamba Tshishimbi, Obrey Chirwa, Pius Buswita na Ibrahim Ajib.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SINGIDA UNITED WAIFUATA JKT TANZANIA NUSU FAINALI AZAM SPORTS FEDERATION Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top