• HABARI MPYA

    Monday, April 23, 2018

    TFF YAZIPONGEZA NGORONGORO HEROES NA SERENGETI BOYS KWA MATOKEO MAZURI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF), Wallace Karia ametoa salamu za pongezi kwa timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) na ile ya chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kwa kufanikiwa kufuzu katika michezo yao iliyochezwa jana huko DR Congo na Burundi.
    Ngorongoro Heroes wamefanikiwa kusonga kwenye raundi ya pili ya kufuzu fainali za Africa za Vijana chini ya miaka 20 zitakazochezwa Niger mwezi Novemba baada ya ushindi wake wa penati 5-6 dhidi ya DR Congo baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya bila kufungana kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Tanzania wakati Serengeti Boys wenyewe wamefuzu hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Vijana ya Cecafa chini ya miaka 17 inayoendelea huko Burundi.
    Karia amesema kufanya vizuri kwa timu hizo za vijana ni faraja kubwa kwa Tanzania na inaonesha namna ambavyo TFF inaendelea kuwekeza kwenye soka la vijana.
    Amesema Vijana hao wa Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys wameonesha jitihada kubwa na wanastahili pongezi kwa jitihada hizo pamoja na jitihada za mabenchi ya ufundi ya timu hizo.
    “Tumepokea matokeo ya Vijana wetu wa Ngorongoro na Serengeti Boys kwa furaha kubwa kwasababu tumekuwa tukihakikisha timu hizi zinapata maandalizi mazuri ambayo yanaonekana uwanjani kwa kupata matokeo mazuri ambayo yanailetea sifa kubwa Tanzania kwa ujumla” alisema Karia.
    Aidha Rais wa TFF Ndugu Karia amesema TFF itaendelea na jitihada kuzipatia maandalizi mazuri zaidi timu hizo ili ziweze kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali yanayowakabili.
    Amesema TFF inajivunia vijana hao ambao wanaonesha mwanga mkubwa na amewaomba watu mbalimbali,Taasisi,makampuni kuunga mkono jitihada za TFF na kuiga mfano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro waliojitokeza na kuisaidia Ngorongoro Heroes katika safari yake ya kwenda DR Congo kwenye mchezo wa marudiano.
    Amemalizia kwa kuwashukuru wote wanaounga mkono jitihada za TFF kuendeleza mpira wa Tanzania huku akiishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais John Pombe Magufuli kwa kuunga mkono na ushirikiano wao kwa TFF.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAZIPONGEZA NGORONGORO HEROES NA SERENGETI BOYS KWA MATOKEO MAZURI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top